Marais na mitindo ya nyimbo wazipendazo

Mwaka wa 2017 rais Uhuru Kenyatta aliwafurahisha wakenya wengi wakiwemo vijana alipo tangaza kwa mara ya kwanza kuwa yeye ni shabiki mkuu wa nyimbo za Reggae. Isitoshe, Kenyatta alisema msanii anayemu enzi zaidi ni gwiji aliyekuwa miongoni mwa waanzilishi wa Reggae, Bob Marley.

Akizungumza na Mbusi na Lion katika mazungumzo ya kipekee, Kenyatta alisema miongoni mwa nyimbo ni Redemption song.

Alisema,

Napenda reggae kabisa lakini yangu ni ile ya zamani, mimi ni mtu ya Bob Marley. Kwanza kabisa ni Stir it up, Redemption Song na Three Little Birds.” Alisema rais.

Licha ya hilo, sio mara moja rais Kenyatta ameonesha mapenzi yake kwa mziki kwani ameonekana akisakata densi kwenye hafla kadhaa bila kuficha. Mojawapo ya hafla anayokumbukwa kwa kusakata densi ni wakati alipokuwa mwenyeji wa rais wa Amerika, Barack Obama katika ikulu ya Nairobi.

Barack Obama

Huku tukizungumzia Barack Obama, rais huyo mstaafu ambaye aliandikisha historia kwa kuwa rais wa kwanza wa Amerika mwenye asili ya ki Afrika, pia anajulikana kwa upendo wake wa muziki.

Inakumbukwa kuwa kabla ya mhula wake wa pili kutamatika, Obama alikuwa na vikao kadhaa na wasanii kutoka nyanja mbali mbali na wasanii wa nchi hiyo huku wengi wao wakiwa wenye asili ya Ki kiafrika.

Hata hivyo mara kwa mara alionekana akizungumzia na kuwataja wasanii aliowapenda au wanaopendwa na wanawe.

Siku ya Jumapili, kupitia mtandao wake wa kijamii, rais huyo wa 44 wa Amerika alichapisha orodha ya nyimbo ambazo pamoja na mkewe, Michelle Obama wamekuwa wakiziskiza katika msimu huu wa joto.

Miongoni mwa nyimbo hizo, ameorodhesha wasanii wa kitambo na wa kisasa. Isitoshe, kuna nyimbo ambazo waweza sema zina mitindo ya haraka na kuna ambazo zina utulivu fulani.

Miongoni mwa nyimbo za wasanii wa kale ni kama;

I've got you under my skin - Frank Sinatra

Don't you worry 'bout a thing - Stevie Wonder

Doo-woop - Lauryn Hill

100 yard daash -Raphael Saadiq

Nyimbo za kizazi kipya ambazo wapenzi hao wawili wanaskiza ni kama;

MOOD 4 EVA Beyonce ft JAY-Z na Childish Gambino

Old Town Road -Lil Nas X’s

Too good - Drake ft Rihanna

Yoweri Museveni

Rais wa Uganda kando na wale wengine, yeye pia ni msanii na tayari amezindua vibao viwili kwa jina; I need another rap, wimbo aliozindua mwaka wa 2011 na pia Yengoma aliozindua mwaka wa 2015.

Nyimbo hizi sana sana yeye huzizindua wiki kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu nchini humo, na huonekana kama njia ya kuwarai wapiga kura wamchague.

Jakaya Kikwete

Mwaka uliopita msanii Diamond Platnumz akiwa katika ziara yake humu nchini alifichua kuwa aliyekuwa rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete aliwahi mpigia simu wakati mmoja kumjulia hali. Hiyo ni ishara tosha kuwa licha ya kuwa rafiki wa karibu wa Diamond, yeye ni mpenzi wa muziki na sanaa.

Diamond alisimulia,

Wakati niko Mwanza nilipokea simu nikaambiwa ananitafuta, nikampigia, nilipompigia akaniuliza maswala ya stage ‘Imekuwaje wakati mmedondoka?’ Nikamwambia  situation vile ilikuwa. Tulikuwa hatujaonana mda mrefu na mzee wangu mzee Kikwete, nilivyo onana naye akanisihi.

Aliongeza,

Sikuwa nimeonana naye kwa mda mrefu tangia alivyokuwa ametoka madarakani lakini mara nyingi alikuwa ananisihi vitu vya maisha, kwa sababu ni mtu ana support sana mziki na pia ni mtu anapenda vijana wake kuwa katika msingi uliokuwa bora.

Jacob Zuma
Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alijulikana duniani kote kwa upendo wake wa muziki. Kama hasakati densi za zama za kale basi alikuwa akiimba kwa mikutano na kongamano mbalimbali.
Zuma anakumbukwa sana kwa kuimba katika mazishi ya hayati, Nelson Mandela mwaka wa 2013.
Mhariri:Davis Ojiambo.