Siku ya uhuru wa vyombo vya habari, Kenya bado inakibarua kuhakikishia wanahabari uhuru wao

JAMBO BREAKING nEWS BANNER
JAMBO BREAKING nEWS BANNER
Na Victor Bwire na Sairin Lupia

Mwezi Mei tarehe 3, huwa siku ya kuadhimisha uhuru wa vyombo vya habari duniani. Ulimwengu unapoadhimisha siku hii muhimu katika sekta ya uanahabari tunafaa kufahamu fika kwamba uhuru wa wananchi kupashwa habari ni swala ambalo linahitaji kutiliwa maanani na kila mmoja wetu.

Katika baadhi ya nchi uhuru wa vyombo vya habari umesalia tu katika maandishi lakini hali halisi ni kwamba vyombo vya habari havina uhuru wa kueleza hali halisi ya mambo katika nchi zao. Wanahabari hutekeleza shughuli zao kwa hofu ya kuadhibiwa na mamlaka husika au hata kuawa.

Ingawa Kenya imepiga hatua kubwa katika kuvipa vyombo vya habari uhuru, bado kuna vikwazo ambavyo vinafaa kushughulikiwa ili kuiondolea sekta hii visiki vinavyo athiri kazi ya uanahabari. Safari ya uhuru wa vyombo vya habari na uandishi kwa jumla nchini Kenya imekuwa ndefu, kutoka enzi ambazo waandishi kama vile Ngungi wa Thiong’o, Maina wa Kinyati, Gitobu Imanyara na wengine wengi kufungwa jela kwa sababu ya uandishi wao ambao ulilenga kufichua uozo katika serikali.

Soma pia;

Enzi hizi wanahabari na waandishi wengine walichukuliwa kama maadui wa serikali na ambao lengo lao kuu lilikuwa kuvuruga mipango ya serikali. Chini ya utawala wa KANU, wanahabari waliteswa kwa kupigwa huku baadhi yao wakiwekwa korokoroni na kutendewa ukatili. Waandishi walilazimika kubadili mbinu ili kuweza kupitisha jumbe zao kwa wananchi. Waandishi wa vitabu na hata watunzi wa mashairi wakatumia vipaji vyao kuonyesha ulimwengu kwamba hata ingawa mkoloni alienda bado Kenya ilikuwa chini ya ukoloni mambo leo.

Katika enzi hii ya karne ya ishirini na moja, bado tunazungumzia uhuru wetu kama waandishi na wanahabari. Bado kuna mengi ya kufanywa na wadau husika kuhakikisha usalama na utendakazi wa wanahabari na waandishi unatiliwa maanani. Waandishi na wanahabari nchini bado wanatishiwa maisha na wale wenye mamlaka, wanasiasa na mabwenyenye kutokana na kazi yao kufichua maovu katika jamii.

Ni wazi kwamba taluuma ya uanahabari nchini Kenya inahitaji ujasiri na uzalendo wa hali ya juu. Mbali na changamoto za kudhulumiwa na mamlaka, wanahabari pia wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi. Wakati huu ambapo taifa linakabiliwa na janga la virusi vya corona asilimia kubwa ya wanahabari nchini Kenya wamepunguziwa mishahara na marupurupu, huku wengine wengi wakilazimika kufanyia kazi nyumbani na ilhali hawana mitandao nyumbani na wale ambao wana mitandao nyumbani hawana uwezo wa kutosha kulipia gharama za mitandao hiyo.

Soma pia:

Baadhi yao wameshambuliwa na polisi watundu, makosa yao yakiwa kutekeleza shughuli zao za uanahabari. Wadau wote katika sekta hii wanafaa kuangazia swala hili kwa uzito unaostahili ili kuimarisha mazingira wanamofanyia kazi wanahabri na waandishi kwa jumla nchini.

Vyombo vya habari hutekeleza wajibu mkubwa sana katika kufahamisha na kuelemisha wananchi kuhusu maswala ya maendeleo, kuangazia utendakazi wa serikali, kufichua maovu serikali ikiwemo sakata mbali mbali na kujuza wananchi kuhusu majanga na kutoa tahadhari.

Viongozi wanafaa kuona sekta hii kama mshiriki mkuu katika ustawi wa taifa wala sio adui mkubwa wa maendeleo. Wanahabari kwa upande wao wana wajibu wa kuripoti taarifa zao bila mapendeleo na kuhakikisha kwamba taarifa zao zote ni sahihi na zimethibitishwa. Vyombo vya habari havifai kutumika kueneza uvumi na propaganda.

Soma pia:

Serikali inafaa kuhakikishia wanahabari usalama wao ili watekeleze shughuli zao bila uoga. Kongole kwa Baraza La Vyombo Vya Habari nchini (Media Council of Kenya), kwa kuwa kinga kwa wanahabari na vyombo vya habari nchini. Baraza hili limepigania sana uhuru na usalama wa wanahabari. Limekuwa katika mstari wa mbele kuwasaidia wanahabari wengi waliokuwa matatani mbali na kupendekeza sheria za kulinda sekta hii muhimu.

Yote haya tisa, la kumi ni kwamba bado kuna mengi ya kufanywa ili kuipa sekta ya habari uhuru kamili wa kutekeza shughui zake bila muingilio wowote. Ule ufa uliokuwepo kati ya serikali na wanahabari ungalipo na unapaswa kuzibwa kwa manufaa ya taifa.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO