Daraja la kuelea majini la Mombasa kukamilika baadaye mwaka huu

Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumamosi alifanya ziara ya shughuli nyingi ya kukagua miradi ya maendeleo katika Kaunti ya Mombasa.

Rais aliaza ziara yake ya siku kutwa katika maeneo ya Liwatoni, Kisiwani Mombasa ambako serikali inajenga daraja linaloelea juu ya maji kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9.

Daraja hilo la umbali wa kilomita 1.2 la kwanza la aina yake katika eneo hili limekamilika kwa asilimia 51 na litakuwa tayari kwa matumizi ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Litakapokamilika, daraja hilo linatarajiwa kupunguza msongamano wa watu katika kivukio cha feri cha Likoni na kuacha feri kutumika tu kubebea magari ya mizigo kati ya Mombasa na Pwani Kusini.

Baada ya kukagua mradi huo wa daraja, Uhuru ambaye alikuwa ameandamana na Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho alivuka na kuingia jengo la kisasa la shughuli za uvuvi la Liwatoni, ambalo linaimarishwa na kuwa bandari ya uvuvi.

Rais alisema ameridhishwa na ukarabati unaoendelea katika kituo hicho cha uvuvi ambacho alisema kitabuni nafasi za kazi kwa vijana na kuimarisha uchumi wa pwani.

Akiwahutubia wafanyabiashara ndogo-ndogo huko Liwatoni, Rais aliwataka wafanyabiashara hao kutumia fursa ya kuwepo kwa miradi hiyo ya daraja na bandari ya uvuvi kustawisha biashara zao.

Rais Kenyatta alimtaka Gavana Joho ashirikiane na mashirika ya serikali ya kitaifa katika kustawisha vibada vya kisasa vya kibiashara ili kuwawezesha wafanyabiashara kunufaika na ongezeko la idadi ya watu watakaokuwa wakitumia daraja hilo mara tu litakapokuwa tayari.

Kwa upande wake, Gavana Joho alisema serikali yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya kitaifa katika utekelezaji wa miradi inayonuiwa kuboresha maslahi ya wakaazi wa Mombasa.