Chama cha Jubilee hakitakuwepo mwaka wa 2022-Adai Caleb Kositany

Muhtasari
  • Mbunge wa Soy Caleb Kositany amekubali kuondolewa kwake kama naibu katibu mkuu wa chama cha Jubilee
  • Caleb Kositany alidai chama cha Jubilee hakitakuwepo mwaka wa 2022
Mbunge Caleb Kositany

Mbunge wa Soy Caleb Kositany amekubali kuondolewa kwake kama naibu katibu mkuu wa chama cha Jubilee.

Hata hivyo alikuwa na mengi ya kusema juu ya uongozi wa chama na mgawanyiko wa hivi karibuni.

Akiwa kwenye mahojiano na runinga ya Citizen baada ya kuondolewa kwake Kositany alidai kuwa chama hicho kinaongozwa chini ya udikteta na wanachama wako gizani kwenye maswala muhimu ikiwa ni pamoja na kuunga mkono muswada wa  BBI.

 

"Jubilee ni hadithi tu iliyosahaulika. Haitakuwepo mnamo 2022. Itashuka kuwa chama kidogo sana kama chama cha KANU," Kositany alisema katika mahojiano.

Nafasi yake Kositany itachukuliwa na mbunge wa Cherangany Joshua Kutuny, Kositany amekuwa mwandani wa naibu rais William Ruto.

 "Makamu mwenyekiti alisema siku nyingine kwamba nitaondolewa leo. Unaweza kuona yeye ndiye mnenaji." Aliongea Kositany.

Katika barua ya Machi 1, katibu mkuu Raphael Tuju alisema uamuzi huo umefanywa baada ya kikao cha Kamati ya Usimamizi ya Kitaifa.