Kang'ata atimua mbio katika mkutano wa DP

Muhtasari
  • Irungu Kang'ata aeleza sababu ya kukimbia katika hafla ya DP Ruto siku ya Jumapili.
  • Kwenye video iliyoenea siku ya Jumatatu, Kang'ata, ambaye alikuwa amevaa suti ya samawati na shati jeupe  alionekana akikimbia kwenda kwa ibada ambayo Ruto alikuwa akihudhuria
kang'ata
kang'ata

Baada ya video yake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii akitimua mbio huku koti lake likipepea kutokana na kasi ya aliokuwa akikimbia, Seneta Irungu Kang’ata ameelezea sabu ya yeye kutimua mbio siku ya Jumapili katika mkutano wa Naibu Rais William Ruto.

Kwenye video iliyoenea siku ya Jumatatu, Kang'ata, ambaye alikuwa amevaa suti ya samawati na shati nadhifu alionekana akikimbilia kwenye ibada ambayo Ruto alikuwa akihudhuria katika kaunti ya Murang’a.

Kang’ata ambaye wiki chache zilizopita alitemwa kutoka wadhifa wa kiranja wa wengi katika Seneti alionekana akichana mbuga na kuacha mlinzi wake nyuma akijikokota kumfikia.

Lakini Jumatatu, Kang'ata alieleza kiini cha yeye kukimbia.

"... nilifika kwa mkutano wa DP nikiwa nimechelewa sana. Nilipata lango limefungiwa na magari. Nilishuka na kukimbia kupita magari yaliyokuwa yakizuia kuelekea kanisani kwasababu hotuba zilikuwa karibu kuisha," alisema.

Kutoaminika kwa Kang'ata huku akishukiwa kuwa kachero wa Tangatanga kulifanya apigwe kalamu kutoka wadhifa wenye ushawishi wa kiranja wa seneti.

Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi alichaguliwa kuchukuwa wadhifa huo.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO