Nitamaliza uhasama uliopi miongoni mwa matawi 3 ya serikali - Koome

Jaji wa mahakama ya rufaa Martha Koome alipofika mbele ya JSC kuhojiwa kuhusu wadhifa wa jaji mkuu, 14/04/2021.
Jaji wa mahakama ya rufaa Martha Koome alipofika mbele ya JSC kuhojiwa kuhusu wadhifa wa jaji mkuu, 14/04/2021.
Image: CHARLENE MALWA

Jaji mkuu mteule Martha Koome ameapa kurejesha umoja na kumaliza uhasama uliopo kati ya mahakama, utawala na bunge 

Koome ambaye yumo ukingoni mwa kuandikisha historia kama jaji mkuu wa kwanza wa kike amewaonya wafisadi kwenye idara ya mahakama kwamba atawageuza kuwa mifano ili wawe funzo kwa wengine.

"Hakuna mwananchi yeyote anayepaswa kulipa afisa wa mahakama ili kupata huduma kwa sababu tunalipwa kutoa huduma," alisema na kuongeza kuwa DCI na EACC watahusika katika mapambano ya kuhakikisha kuwa mahakama haina ufisadi.

Aliiambia kamati kuwa amewatumikia Wakenya sawasawa ikiwa ni pamoja na kumwakilisha kiongozi wa upinzani Raila Odinga kama wakili kiongozi wakati alipozuiliwa bila kesi na utawala wa marehemu Rais Daniel Moi.

"Ninawahudumia Wakenya kwa kujitolea kabisa kutoka kwa kina cha moyo wangu na jinsia yangu au kule ninakotokea hakunizuii."

Katika onyesho lingine la kuachana na mtangulizi wake, Koome alisema hatakuwa na shida ya kufika mbele ya Kamati za Bunge, jambo ambalo Maraga hakufanya wakati wa miaka yake mitano ya uongozi.