YAPI YALIYOMKUMBA KIBET?

Mwanafunzi aliyevamia ikulu sasa ajitambulisha kuwa nabii tajiri

Brian Kibet Bera amekamilisha kujenga kijumba cha matope anachodai atakodisha shilingi mia tano kila mwezi.

Muhtasari

•Kibet anajitambulisha kuwa Nabii wa Mungu na kuwahubiria Wakenya kwenye Facebook

•Wakenya wameagiza wasamaria wema kumsaidia kupata huduma za mtaalamu wa kiakili

Brian Kibet Bera
Brian Kibet Bera
Image: Facebook

Kijana aliyekamatwa kwenye majaribio ya kuvamia ikulu na kisu mwaka jana, Brian Kibet Bera  ametangaza kuwa yeye sasa ni tajiri.

Hii ni baada ya barubaru huyo kukamilisha kijumba cha matope anachotangaza kuwa atakodisha shilingi mia tano kwa mwezi.

Inadaiwa kuwa huenda kijana yule ana tatizo la kiakili baada yake kuonekana akijiita nabii kwenye mtandao wa Facebook huku akivuta sigara, madai ambayo baadhi ya marafiki wake wamekanusha.

Chapisho la Kibet
Chapisho la Kibet
Image: Hisani

Kibet amekuwa akitumia ukurasa wake kuwahubiria Wakenya na kuwapa simulio za tukio alizopitia kisha kuomba sadaka kupitia nambari ya Mpesa aliyoweka pale, jambo ambalo limeibua gumzo sana mitandaoni.

Kupitia jumbe alizochapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook, Kibet amesema kuwa amekuwa akitoa dhabihu kwake Mungu na kwa namna hiyo Mungu akamtendea makuu.

“Kweli hata mbwa hungoja chakula kianguke toka mezani ndiyo wakule. Mbona nizihifadhi pesa za ziada nilizo nazo, naweza fungwa jela leo. Itakuwa pesa ya nani wakati ule?” Brian ameandika huku akidai kuwa amekuwa akitembelea mayatima, wajane, wasio na makwao na walala hoi.

Kibet kwa muda wa hivi majuzi amekuwa akitumbuiza Wakenya kwenye mtandao wa Facebook na chapisho za utata huku Wakenya wa nia njema wakiomba wasamaria wema kumsaidia Kibet kwani anaonekana mwenye kuhitaji huduma za mtaalamu wa kiakili.