Karibu watu 100 wauawa katika shambulio Burkina Faso

Wanajeshi wa Burkina Faso wanajitahidi kudhibiti ghasia za wanamgambo
Wanajeshi wa Burkina Faso wanajitahidi kudhibiti ghasia za wanamgambo
Image: bbc

Wanaume waliojihami wamewaua karibu watu 100 katika shambulio kwenye kijiji kimoja kaskazini mwa Burkina Faso, Rais Roch Kabore amesema.

Wakati wa shambulio hilo la usiku dhidi ya Solhan, nyumba na soko pia ziliteketezwa, shirika la habari la Reuters linanukuu taarifa ya serikali.

Hakuna kundi lolote lilitangaza kuhusika na shambulio hilo.

Lakini mashambulio kutoka wanamgambo wakijihadi yameongezeka nchini humo, hasa maeneo yanayopakana na Niger na Mali.

Rais Kabore ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa akisema, katika ujumbe wa Twitter, kwamba "lazima tuungane dhidi ya maadui".

Vikosi vya usalama kwa sasa vinawatafuta waliohusika katika shambulio hilo, aliongeza.

Katika shambulio lingine la usiku wa Ijumaa, watu 14 waliripotiwa kuuawa katika kijiji kingine, karibu kilomita 150 kaskazini mwa Solhan.

Mwezi uliyopita, watu 30 walifariki katika shambulio lingine mashariki mwa Burkina Faso.

Nchi hiyo inakabiliwa na mzozo mkubwa wa usalama, sawa na majirani zake, kwani makundi yaliojihami yanashambulia na kuwateka watu katika eneo hilo.

Mnamo mwezi Mei, jeshi la Burkina Faso lilizindua oparesheni kubwa ya kudhibiti mashambulio ya wanamgambo.

Licha ya hatua hiyo, vikosi vya usalama bado vinajizatiti kuzuia ghasia ambazo zimesababisha zaidi ya watu milioni moja kutoroka makwao katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mataifa kadhaa masikini zaidi duniani yanapakana na jangwa la Sahara.

Ukanda huo unajulikana kama "Sahel", neno la Kiarabu linalomaanisha "pwani".

Mali, Chad, Niger, Burkina Faso na Mauritania zinaunda nchi za Sahel na zote zinakabiliwa na mashambulio kutoka kwa wanamgambo.

Sehemu za ukanda huo zinakumbwa na ukame, umaskini, ukosefu wa ajira na ufisadi.