"Wakenya hawana haja na miungano ya kisiasa" Ruto akosoa miungano ya kisiasa

Naibu rais William Ruto amesema kuwa shida kubwa inayowakumba Wakenya sio tofauti za kikabila ila ni kuzorota kwa uchumi.

Muhtasari

•Ruto alisema kuwa anafahamu kuwa miungano ambayo inaundwa ni ya kujaribu kumzuia kutwaa kiti cha urais mwaka ujao.

•Hata hivyo, naibu rais aliwahakikishia Wakenya kuwa miungano hiyo ambayo alisema ni ya kikabila haitamzuia kuingia ikulu kwani amejipanga.

•Ruto aliwakashifu viongozi wanaojiandaa kuungana  kwa madai kuwa wanadanganya Wakenya kuwa  wakiungana uchumi utaboreshwa. Alisema kuwa Wakenya hawana haja na miungano hiyo ila haja yao ni namna ya kuinua uchumi.

Naibu rais William Ruto akihutubia wananchi katika kaunti ya Machakos siku ya Jumapili
Naibu rais William Ruto akihutubia wananchi katika kaunti ya Machakos siku ya Jumapili
Image: GEORGE OWITI

Naibu rais William Ruto ameendelea kukosoa muungano wa Jubilee na vyama vingine.

Ruto amewasihi viongozi kuacha kuwadanganya wananchi kuwa miungano ya kisiasa ndiyo suluhu ya matatizo yanayokumba nchi ya Kenya.

Akihutubia wananchi katika kaunti ya Machakos siku ya Jumapili, Ruto alisema kuwa anafahamu kuwa miungano ambayo inaundwa ni ya kujaribu kumzuia kutwaa kiti cha urais mwaka ujao.

"Nataka niwaulize marafiki zangu viongozi kwa sababu nimeona wanasiasa wengi wanasema wanataka kuungana ili kukabiliana na mimi na mahustlers. Nataka niwaambie saa zile mnajianga kuungana, hawa wananchi wa Kenya hawana haja na miungano ya viongozi. Hawataki kujua mpinzani wenu ni nani. Wananchi wanataka vile wataungana wenyewe washughulike ili wenye hawana kazi wapate" naibu rais alisema.

Ruto alitupilia mbali miungano hiyo na kusema kuwa nia kuu ya viongozi kuungana ilikuwa ili kukabiliana naye kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Hata hivyo, naibu rais aliwahakikishia Wakenya kuwa miungano hiyo ambayo alisema ni ya kikabila haitamzuia kuingia ikulu kwani amejipanga.

"Hawa watu wanajipanga lakini hata mimi nimejipanga. Nimejipanga na mahustlers. Hawa wangwana watakiona, watajua hawajui" Rutoa alisema.

Ruto alisisitiza kuwa miungano hiyo ilikuwa inaundwa kwa misingi ya kikabila ila sio kutafuta suluhu ya matatizo yanayokumba taifa.

Alisema kuwa shida kubwa inayowakumba Wakenya sio tofauti za kikabila ila ni kuzorota kwa uchumi.

"Nauliza nyinyi, viongozi wakiungana au wasipoungana, ni siasa na ukabila unataka ama ni uchumi ubadilike wewe upate kazi  na pesa kwa mfuko? Shida ni ukabila ama ni uchumi?.. si ni uchumi? Uchumi ukibadilika mpate kazi na pesa, wewe uko na shida na mtu wa kabila nyingine? si bora upate kazi, ufanye biashara na upate pesa mfukoni" aliendelea kusema.

Ruto aliwakashifu viongozi wanaojiandaa kuungana  kwa madai kuwa wanadanganya Wakenya kuwa  wakiungana uchumi utaboreshwa. Alisema kuwa Wakenya hawana haja na miungano hiyo ila haja yao ni namna ya kuinua uchumi.

"Kwa hivyo hao wangwana tunawaambia, unganeni ikiwa mnataka kuungana, kabilianeni na wapinzani wenu vile mnataka. Lakini hapa chini, wananchi  wanangojea sera ambazo zitawapatia kazi na biashara na iweke pesa kwa mifuko yao" alisema Ruto.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya maafisa wa chama cha Jubilee na kile cha ODM kukutana katika mkahawa mmoja jijini Nairobi na kushiriki majadiliano ya kuunda msingi wakiwa na matumaini ya kuteua mgombeaji kiti mmoja atakayeungwa mkono kwenye chaguzi kuu.