"Hata Mungu hapendi mtu asiye baridi wala moto" Ngunjiri amtaka Ruto kujiuzulu

Mbunge wa Nyeri, Ngunjiri Wambugu amemwambia naibu rais William Ruto kuwa kujiondoa kwake hakutafanya chama cha Jubilee kufa.

Muhtasari

•Wambugu ambaye anajitambulisha na mrengo wa ‘Kieleweke’  amemtaka naibu rais William Ruto kujiondoa kutoka chama cha Jubilee na kujiunga rasmi na UDA

•Ametoa hisia hizi huku Ruto akionekena kama kwamba anatayarisha Wakenya kwa kuondoka kwake kirasmi kutoka chama cha Jubilee kutokana na matamshi yake ya hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii.

Mbunge wa Nyeri, Ngunjiri Wambugu
Mbunge wa Nyeri, Ngunjiri Wambugu
Image: The Star

Huku mvutano mkubwa ukiendelea kushuhudiwa katika chama tawala cha Jubilee, sasa mbunge wa Nyeri, Ngunjiri Wambugu amemtaka naibu rais William Ruto kujiondoa kwenye chama hicho na kujiunga rasmi na chama cha UDA.

Wambugu ambaye anajitambulisha na mrengo wa ‘Kieleweke’ amemwambia Ruto kuwa kujiondoa kwake hakutafanya chama cha Jubilee kufa.

Mtu amwambie Ruto kuwa kuondoka kwake kutoka chama cha Jubilee hakumaanishi kuwa chama kitakufa. Aligura chama cha ODM na bado kinaendelea . Kwa hakika, vyama hivyo viwili vinaendelea vyema tangu aondoke” Ngunjiri aliandika kwenye mtandao wa Facebook.

Alikuwa anatoa hisia zake kufuatia matamshi ya naibu rais kwenye mitandao ya kijamii akidai kuwa kuvunjwa kwa chama cha Jubilee kulikuwa kunatengenezea njia vyama vya ‘kikabila’ ambavyo vimo kwenye muungano wa NASA.

“Kwa hivyo kuharibiwa na kusahaulika kwa chama cha kitaifa cha Jubilee kulifanyika ili kutengenezea njia uungaji mkono wa vyama vya maeneo na kikabila vilivyo ndani ya NASA? Vile chama cha Jubilee kwa sasa kimesambaratika, si ni haki kwa wale ambao hawawezi kutoshea kwenye vyama vya kikabila kuunda UDA kama chama mbadala cha kitaifa? Ama?” alikuwa ameandika Ruto kwenye akaunti yake ya Twitter.

Wambugu amemwagiza naibu rais kujiuzulu na kujiunga na UDA mara moja “kwani hata Mungu hapendi watu ambao si moto wala baridi.”

Amesema kuwa Ruto atakuwa anafuata katiba iwapo atakubali kujiuzulu.

Wambugu pia amesisitiza kuwa kufikia mwisho wa utawala wa Jubilee, chama hicho kitakuwa kimezoa alama nyingi kwa upande wa maendeleo nchini Kenya.

Hasira yake inatokana na ukweli wa kuwa ifikapo 2022, sisi ambao tuko kwenye chama cha Jubilee tutakuwa tunajivunia maendeleo makubwa ndani ya miaka kumi ya utawala ilhali yeye na wenzake wa UDA watakuwa wanapeana ahadi kuhusu yale watafanya iwapo watachaguliwa” Wambugu alisema.

Mbunge huyo kutoka eneo la mlima Kenya amekuwa mkosoaji nambari moja wa naibu rais William kwa muda sasa. Ameonekana kutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kumkashifu na kumkejeli Ruto tangu mwanzo wa vita ndani ya chama tawala.

Ametoa hisia hizi huku Ruto akionekena kama kwamba anatayarisha Wakenya kwa kuondoka kwake kirasmi kutoka chama cha Jubilee kutokana na matamshi yake ya hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii.