MASAIBU YA JUBILEE

Waiguru adai mabadiliko katika chama cha Jubilee

"Mvua imetupiga. Bahati inatupungukia. Kujichunguza vikali kunahitajita" Gavana Waiguru asema

Muhtasari

•Waiguru amekiri kuwa hali katika chama chama cha Jubilee sio nzuri.

•Waiguru pia ameagiza chama hicho kukubali kufungua milango yake kwa watu kuingia na kurudi tena.

Gavana Waiguru akizungumza mwakani 2019
Gavana Waiguru akizungumza mwakani 2019
Image: Hisani

Gavana wa Kirinyaga, Anne Mumbi Waiguru ametaka chama tawala cha Jubilee kuangazia mabadiliko tunapokaribia uchaguzi mkuu wa 2022.

Kupitia mtandao wa Facebook, gavana huyo wa muhula wa kwanza amekiri kuwa hali katika chama hicho sio nzuri.

"Mvua imetupiga. Bahati inatupungukia. Kujichunguza vikali kunahitajita"  Gavana Waiguru alisema.

Gavana huyo ambaye aliponea chupuchupu kutimuliwa mwaka mmoja uliopita amesema kuwa ni sharti chama cha Jubilee ambacho alichaguliwa kupitia kuelewa kuwa muktadha wa siasa nchini umebadilika na kuwa vijana wanachukua usukani kwenye upigaji kura.

"Tunapoelekea 2022 ni sharti chama kielewe kuwa tuko katika mazingira tofauti na ilivyokuwa miaka kumi iliyopita. Upigaji kura unatawaliwa na vijana. Lazima mikakati yetu iwiane na nyakati tulizo kwa hivyo lazima tukumbatie mawazo mapya na njia mpya za kutekeleza siasa. Tunahitaji Jubilee iliyotiwa nguvu mpya inayoangazia Kenya kwa njia tofauti" Gavana Waiguru alisema.

Waiguru pia ameagiza chama hicho kukubali kufungua milango yake kwa watu kuingia na kurudi tena.

"Mambo mengi ya usoni yamefungwa na hatma ya chama na lazima turejeshe maono, utukufu na hadhi ya chama au tukabiliane na matokeo yatabirikayo" Waiguru alimalizia kwa kusema.

Kwa muda sasa, hali haijakuwa hali tena katika chama hicho kinachoongozwa na rais huku baadhi ya viongozi waliochaguliwa na tikiti ya chama hicho wakijitenga kabisa na kukizungumzia vibaya chama hicho.

Mvutano katika chama hicho ulianza kushuhudiwa  baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 haswa baada ya salamu za 'handshake' kati ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM, Raila Odinga.

Naibu rais na wafuasi wake walihisi kana kwamba wametemwa nje jambo ambalo liliwafanya kuanza kuwa wapingaji wakuu wa chama hicho.

Jubilee imekuwa ikiandikisha matokeo duni kwenye chaguzi ndogo zilizofanyika hivi majuzi huku ikikosa kunyakua kiti chochote kwenye chaguzi ndogo za Juja, Bonchari na Rurii ambazo zilifanyika mwezi uliopita.

Matokeo hayo hafifu yamepelekea baadhi ya wanachama kupendekeza mabadiliko kwenye chama.