Vyama vya kisiasa, raia waonywa vikali dhidi ya mashambulizi yanayolenga wanahabari

Hii inafuatia tukio lililoibuka Jumamosi, Julai 10 ambapo wanahabari waliokuwa wamehudhuria hafla ya kisiasa maeneo ya Mathare kushambuliwa, kuumizwa na kuibiwa vifaa vyao na kikundi cha vijana.

Muhtasari

•Baraza la vyombo vya habari nchini Kenya(MCK) limewapea onyo kali raia wanaoshambulia wanahabari katika mikutano ya kisiasa.

•Katika tukio hilo, wanahabari kutoka The Star, Standard Group, Citizen TV, NTV, KBC,  mwandishi wa habari wa kimataifa kutoka runinga ya Equatoria TV Kaka Juma na wengine walipigwa na kuibiwa na vijana ambao walivamia gari lao na kuwaamrisha kuwapa pesa walizokuwa nazo.

Wanahabari
Wanahabari
Image: Maktaba

Baraza la vyombo vya habari nchini Kenya(MCK) limewapea onyo kali raia wanaoshambulia wanahabari katika mikutano ya kisiasa.

Kupitia ujumbe wa kuchapishwa ambao ulitolewa siku ya Jumapili, MCK imevihimiza vyama vya kisiasa kushawishi wafuasi wao kuzingatia sheria na amani katika mikutano ya kisiasa.

"Tungependa kuonya raia dhidi ya kushambulia wanahabari kwani huo ni ukiukaji mkubwa wa haki za kujieleza, za vyombo vya habari na upatikanaji wa habari zilizopeanwa na katiba katika kipengele cha 33, 34, 35 mtawalia na sheria ya baraza la vyombo vya habari ya 2013" MCK iliandika.

Hii inafuatia tukio lililoibuka Jumamosi, Julai 10 ambapo wanahabari waliokuwa wamehudhuria hafla ya kisiasa maeneo ya Mathare kushambuliwa, kuumizwa na kuibiwa vifaa vyao na kikundi cha vijana.

Katika tukio hilo, wanahabari kutoka The Star, Standard Group, Citizen TV, NTV, KBC,  mwandishi wa habari wa kimataifa kutoka runinga ya Equatoria TV Kaka Juma na wengine walipigwa na kuibiwa na vijana ambao walivamia gari lao na kuwaamrisha kuwapa pesa walizokuwa nazo.

"Kesi hiyo iliripotiwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga na uchunguzi unaendelea" MCK ilisema.

MCK imewataka polisi kufanya hara katika uchunguzi wao na kuwapa wahalifu husika adhabu ifaayo.

"Wanahabari ni wajumbe na hawafai kushambuliwa kutoka pande yoyote. Baraza linachukulia jambo hilo kwa uzito  na tunaagiza polisi kuharakisha uchunguzi wao na kuwaadhibu wahalifu ifaavyo kisheria" MCK ilisema.