Jamaa akamatwa kwa kudukua mitandao ya IEBC, kupata maelezo ya watu 61,617 na kuyatumia kuiba mamilioni

Alipatikana na kitita kikubwa cha kadi za simu za Safaricom, Airtel na Telkom

Muhtasari

•Kijana huyo ambaye anaripotiwa kuwa alikuwa mfanyakazi wa kampuni moja ya huduma za simu nchini Kenya alinaswa na wapelelezi wa uhalifu wakishirikiana na wapelelezi wa ultapeli katika kampuni ya Safaricom na walinzi wa chuo kikuu cha JKUAT akiwa maeneo ya Juja.

•Kwenye tukio moja, mshukiwa pamoja na wenzake wanaripotiwa kutapeli ajenti wa MPESA pesa ambazo zilikuwa kwa akaunti yake ya mkopo .

Image: TWITTER//DCI

Polisi wanamzuilia jamaa mmoja anayedaiwa kuwa mmoja wa kikundi cha wahalifu ambao walidukua mitambo ya IEBC na kupata maelezo ya watu 61,617 kutoka kaunti moja maeneo ya Magharibi mwa Kenya wakiwa na njama ya kuwaibia.

Kiprop, 21, pamoja na wenzake ambao waliweza kutoroka mtego wa polisi wanadaiwa kuibia Wakenya  mamilioni ya pesa kupitia ulaghai wa kimitandao.

Kijana huyo ambaye anaripotiwa kuwa alikuwa mfanyakazi wa kampuni moja ya huduma za simu nchini Kenya alinaswa na wapelelezi wa uhalifu wakishirikiana na wapelelezi wa ultapeli katika kampuni ya Safaricom na walinzi wa chuo kikuu cha JKUAT akiwa maeneo ya Juja. 

Mshukiwa huyo ambaye anaaminika kuwa mmoja wa genge la watapeli wa kimitandao ambao wamekuwa wakiwaibia Wakenya wakijifanya kuwa wasaidizi wa huduma za simu alipatikana na kitita kikubwa cha kadi za simu za Safaricom, Airtel na Telkom.

Kikundi hicho kinadaiwa kutumia maelezo ya watu ambao walipata kwenye mitandao ya IEBC  kuwatapeli  maajenti wa huduma mbalimbali za simu wakidai kuwa wamiliki rasmi wa simu fulani ili kuweza kupata kibali cha kutumia akaunti za kimitandao za wahasiriwa.

Kwenye tukio moja, mshukiwa pamoja na wenzake wanaripotiwa kutapeli ajenti wa MPESA pesa ambazo zilikuwa kwa akaunti yake ya mkopo .

Inadaiwa kuwa mshukiwa alijifanya msaidizi wa Safaricom  akapigia mhudumu mmoja wa MPESA  na kumdanganya abonyeze nambari fulani alizompatia.

Ajenti huyo alifanya kama alivyoagizwa ila kabla hajagundua kuwa pesa alizokuwa nazo kwenye akaunti zilikuwa zimeibiwa.