Mwanamke kushtakiwa kwa kosa la kuua mwanawe wa miaka 10 kufuatia mzozo wa shilingi 100 Kitui

Atashtakiwa mnamo Novemba 9 mwakani.

Muhtasari

•Ripoti za polisi zinaashiria kuwa Mbosya alimpiga mwanawe hadi kifo baada ya kumshutumu kuwa alikuwa ameiba pesa zake shilingi 100 ambazo ni mshahara wake wa siku moja.

•Upande wa mashtaka ukiwakilishwa na wakili Christine Kabaale uliarifu mahakama kuwa mshukiwa tayari alikuwa amefanyiwa vipimo vya kiakili katika hospitali ya Mathari na matokeo yakabaini kuwa ako na akili timamu.

court
court

Habari na Musembi Nzengu

Mwanamke mmoja ambaye anadaiwa kuua mwanawe wa miaka kumi kwa kuchukua na kutumia pesa zake shilingi 100 atashtakiwa mnamo Novemba 9 mwakani.

Mary Mbosya Simon anatuhumiwa kumuua mwanawe Aaron Mwau Mulani mnamo Septemba 24 katika kijiji cha Kaveta, kaunti ndogo ya Kitui ya kati.

Ripoti za polisi zinaashiria kuwa Mbosya alimpiga mwanawe hadi kifo baada ya kumshutumu kuwa alikuwa ameiba pesa zake shilingi 100 ambazo ni mshahara wake wa siku moja.

Mbosya alipoenda kudai pessa zake kutoka kwa mwajiri wake aliarifa kuwa mwanawe alikuwa amezichukua tayari. Hapo akajawa na hasira na akaenda kuagiza mwanawe azitoe kwa fujo.

Mulani ambaye alikuwa mwanafunzi katika shule ya msingi ya Isaangwa alipokosa kutoa pesa zile, Mbosya alimfunga kwa kamba na akaanza kumpa kichapo cha mbwa kwa kutumia panga butu.

Ripoti za polisi ziliashiria kuwa Mbosya alimgonga mwanawe kichwani kwa upanga ule na kusababisha kifo chake.

Siku ya Alhamisi hakimu wa mahakama ya Kitui Maureen Kimani aliamuru Mbosya asomewe mashtaka ya mauaji dhidi yake.

Upande wa mashtaka ukiwakilishwa na wakili Christine Kabaale uliarifu mahakama kuwa mshukiwa tayari alikuwa amefanyiwa vipimo vya kiakili katika hospitali ya Mathari na matokeo yakabaini kuwa ako na akili timamu.

Kuona kuwa mshukiwa ana uwezo wa kujibu mashtaka, hakimu Kimani aliamuru ashtakiwe mapema mwezi ujao.