Polisi wachunguza kifo tatanishi cha msimamizi wa klabu Kitale

Muhtasari

•Kulingana na Meneja wa klabu hiyo Bw. Brian Siambe, marehemu alikuwa aliingia kwenye baa hiyo akiwa tayari amelewa mwendo wa saa mbili asubuhi lakini hakuagiza kiburudisho chochote.

crime scene
crime scene

Polisi katika kituo cha polisi cha Kitale wanachunguza kifo cha ghafla cha msimamizi katika kilabu cha Kitale jana Ijumaa.

Afisa wa Upelelezi wa Jinai wa Kaunti (CCIO) Bw. Francis Kihara alithibitishia Shirika la Habari la Kenya (KNA) kwamba Bw. James Abdi Karrim, mwenye umri wa miaka 34, alipatikana amefariki ndani ya Club Touch Night Club.

Kulingana na Meneja wa klabu hiyo Bw. Brian Siambe, marehemu alikuwa aliingia kwenye baa hiyo akiwa tayari amelewa mwendo wa saa mbili asubuhi lakini hakuagiza kiburudisho chochote.

"Badala yake alikaa kwenye kochi ambapo alijinyoosha na ikadhaniwa kuwa amelala," alisema Siambe.

Siambe aliongeza wafanyakazi katika klabu hiyo walipata wasiwasi wakati Karrim aliposhindwa kuamka na kuondoka kwenye jumba hilo hata baada ya watu wengine wote kuondoka hadi saa 3 asubuhi.

"Tulitoa tahadhari kabla ya maafisa wa usalama kutoka Kituo cha Polisi cha Kitale kufika na kuthibitisha kuwa amefariki," meneja wa klabu hiyo alisema.

Kulingana na Kihara, uchunguzi wa awali ulionyesha mwili huo haukuwa na jeraha linaloonekana. "Maafisa wa eneo la uhalifu walijifunza kutoka kwa dada wa marehemu, Bi. Fardosa Ali ambaye alikuwa katika eneo la tukio kwamba alikuwa na historia ya mashambulizi ya pumu," aliongeza Kihara.

Mwili huo ulipelekwa katika Hospitali Ndogo ya Kaunti ya Trans Nzoia kwa uchunguzi wa maiti CCIO aliihakikishia familia na wananchi uchunguzi wa kina utafanyika ili kubaini chanzo hasa cha kifo hicho, ambacho kimezua taharuki ndani ya klabu hiyo.

(Utafsiri: Samuel Maina)