Jamaa aua mkewe baada ya kuangalia simu yake na kuona ujumbe tatanishi uliotumwa na jamaa mwingine Kakamega

Muhtasari

•Edwin Okoth Owino (27)  anadaiwa kupiga mke wake vibaya hadi kifo baada ya kuona ujumbe wa simu ambao alikuwa amepokea kutoka kwa jamaa mwingine.

•Ili kuficha ukweli kuhusu kilichokuwa kimetendeka pale, mshukiwa alikuwa ametengeneza eneo la tukio ikae kama kwamba marehemu alikuwa amekunywa sumu.

crime scene 1
crime scene 1

Polisi katika kaunti ya Kakamega wanazuilia jamaa mmoja anayeripotiwa kuua mkewe baada ya kumshuku kuwa na mpango wa kando.

Edwin Okoth Owino (27)  anadaiwa kupiga mke wake vibaya hadi kifo baada ya kuona ujumbe wa simu ambao alikuwa amepokea kutoka kwa jamaa mwingine.

Maafisa wa DCI wameripoti kwamba Okoth alijaribu kuficha matendo yake kwa kudanganya kuwa mkewe alikuwa amejitoa uhai.

Okoth anaripotiwa kuelekea  katika kituo cha polisi cha Musanda, eneo la Mumias alfajiri ya Ijumaa na kupiga ripoti kuhusu kifo cha ghafla cha mke wake.

Hata hivyo afisa aliyekuwa amesimamia kituo hicho hakutosheka na simulizi ya mshukiwa na akaagiza maafisa kadhaa wamfuate hadi nyumbani kwake ili kuthibitisha madai yake.

Polisi wale walipofika kwenye eneo la tukio walipata mwili wa mwanadada huyo wa miaka 24 ukiwa  umejaa ishara za kupigwa kila mahali.

Ili kuficha ukweli kuhusu kilichokuwa kimetendeka pale, mshukiwa alikuwa ametengeneza eneo la tukio ikae kama kwamba marehemu alikuwa amekunywa sumu.

Polisi walipokuwa wanafanya uchunguzi zaidi pale nyumbani kwa mshukiwa, mwanadada wa miaka 16 aliyeponea chupu chupu kuandamana na rafikiye kaburini usiku wa Alhamisi alijitokeza na kufichua ukweli wote.

Alieleza kwamba mshukiwa aliona ujumbe ukiingia kwa simu ya mkewe mida ya saa nne unusu  usiku na kushuku kwamba ulikuwa umetumwa na mpango wa kando.

Baada ya ujumbe huo mshukiwa alienda kuita mwanadada huyo (msimulizi) ambaye aliamini kuwa ni rafiki wa dhati wa mkewe na aliporudi kwake akachukua kipande cha mti na kukitumia kuwapiga wote wawili.

Rafiki huyo wa mkewe aliweza kutoroka baada ila marehemu akaaga kutokana na majeraha mabaya ambayo alipata kutokana na kichapo alichopata.

Uchunguzi zaidi unaendelea huku Okoth akiwa kizuizini akisubiri kushtakiwa kwa kosa la mauaji