Mwanasiasa wa Busia akamatwa kwa kupiga raia risasi katika mkutano wa Ford Kenya

Muhtasari

•Osore anaripotiwa kufyatua bastola yake kiholela na kumjeruhi Maurice Wafula baada ya kuzozana na mjumbe mmoja katika mkutano huo.

Arrest
Arrest

Polisi katika eneo la Lang'ata wamemkamata mwanasiasa mmoja anayedaiwa kumpiga mtu risasi wakati wa mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe wa chama cha Ford Kenya katika ukumbi wa Bomas of Kenya siku ya Alhamisi.

Kupitia taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa, tume ya huduma kwa polisi nchini (NPS)  imetangaza kwamba mwenyekiti wa chama cha Ford Kenya katika kaunti ya Busia Emmanuel Osore anazuiliwa kufuatia tukio hilo lililotokea siku ya Alhamisi.

Osore anaripotiwa kufyatua bastola yake kiholela na kumjeruhi Maurice Wafula baada ya kuzozana na mjumbe mmoja katika mkutano huo. 

"Emmanuel Osore alizozana na mmoja wa wajumbe. Kwa hasira akatoa bastola yake na kufyatua risasi kiholela na kujeruhi Maurice Wafula" NPS imesema.

Osore atashtakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya bunduki ya kibinafsi.

NPS imeagiza raia ambao wamepewa leseni za kumiliki bunduki wawajibike haswa katika msimu huu wa kampeni.

Mkutano wa wajumbe wa kitaifa wa FORD-K ulikuwa umeitishwa na mrengo wa chama hicho unaoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang'ula. 

Awali, mrengo wa Ford Kenya unaoongozwa na Mbunge wa Tongaren Eseli Simiyu ulitangaza kusimamisha mkutano wao kufuatia agizo la Mahakama ya kutatua mizozo ya vyama vya Kisiasa.