Hiyo ni joto ya kuhitimu!Ngunjiri Wambugu atetea maafisa wapya wa GSU waliojirekodi wakisherehekea

Muhtasari

•Kulingana na mbunge huyo wa muhula wa kwanza, ni kawaida kwa binadamu yeyote kusherehekea kwa njia tofauti wanapomaliza mafunzo yoyote magumu kama waliyoyapitia  maafisa hao wapya.

Image: FACEBOOK// NGUNJIRI WAMBUGU

Mbunge wa Nyeri Ngunjiri Wambugu  amekosoa tume ya huduma ya polisi (NPS) kwa kulaani tabia na matamshi ya kundi la maafisa wapya wa kitengo cha GSU ambao walijirekodi wakisherehekea kwa kumaliza mafunzo na video yao kusambaa mitandaoni.

Akitoa hisia  zake kupitia ukurasa wake wa Facebook, Wambugu amesihi NPS kuwaacha maafisa hao wenye umri wa ujana kusherehekea kuhitimu kwao na kutowaadhibu kwa matendo yao.

Kulingana na mbunge huyo wa muhula wa kwanza, ni kawaida kwa binadamu yeyote kusherehekea kwa njia tofauti wanapomaliza mafunzo yoyote magumu kama waliyoyapitia  maafisa hao wapya.

"Patieni wahitimu wapya wa GSU amani! Vijana walioonyeshwa kwenye klipu hiyo wamekuwa wamefungiwa kwa miezi mingi katika programu ya mafunzo  ambayo huwageuza kutoka kuwa Wakenya wa kawaida na kuwa wanajeshi. Binadamu yeyote ambaye anapitia mchakato kama huo atapumua mara tu watakapomaliza. Watapiga kelele na nduru. Naamini inatokea katika hafla yoyote ya kuhitimu kutoka kwa mafunzo yoyote ya ulinzi mkali" Wambugu aliandika.

Amesema hatua ya maafisa hao kurekodi video wakisherehekea na kuipakia mitandaoni ni kwa sababu wao ni vijana kutoka kizazi cha sasa ambao wana mazoea ya hurekodi kila tukio maishani. 

" Hatuwezi kuwaadhibu kwa hilo. Wape vijana mapumziko. Hiyo ni joto ya kuhitimu na itaisha haraka sana hapa nje. Zaidi ya hayo hawakusababisha madhara yoyote kwa yeyote. Ni watoto tu ambao walipitia mafunzo magumu" Alisema Wambugu.

Siku ya Alhamisi idara ya polisi ilitoa taarifa ikilaani vikali tabia na matamshi ya maafisa wapya wa GSU ambao walijirekodi wakichangamka baada ya kumaliza mafunzo na klipu yao kusambaa kote mitandaoni.

NPS ilisema matamshi ya maafisa hao ni ya kusikitisha kwani wahitimu wote walipitia mafunzo muhimu kuhusiana na kanuni za kidemokrasia za polisi kwa lengo la kuwafanya maafisa wasikivu na wanaowajibika katika kazi yao ya kuhudumia umma.

Polisi walitoa hakikisho kuwa uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo unaendelea na hatua mwafaka zitachukuliwa baada ya ukaguzi wa ndani kukamilika.

Katika video inayoenea sana mitandaoni, kikundi kidogo cha makurutu wa GSU  wenye umri wa ujana kinaoneka kuchangamka wanaposherehekea kukamilisha mafunzo yao.

Maafisa hao wanaonekana wakisakata densi  za kisasa kusherehekea kufuzu kwao huku wakijigamba kuhusu ukali wao wanapojiandaa kuanza kuhudumia taifa.

"Ndio hiyo, tiushamaliza.. mabang'a. Tunawakilisha, hii ni red barret.. tunakuja nje. Apana tambua. Hawa ni wale wazii, wabaya. Pa! Pa! Pa!" Maafisa hao wangesikika wakisema.

Wakenya ikiwemo viongozi wameendelea kutoa hisia tofauti kuhusiana na video hiyo baadhi yao  wakipendekeza adhabu kwa maafisa husika huku wengine wakiwatetea.