Idara ya polisi yalaani matamshi ya maafisa wapya wa GSU katika video inayosambaa mitandaoni

Muhtasari

•NPS  imesema tabia ya makurutu hao kama ilivyoashiriwa kwenye video inayoenezwa mitandaoni haikubaliki na haiambatani na maadili ya kitengo cha GSU wala polisi kwa ujumla.

•NPS imetoa hakikisho kwamba uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo unaendelea na hatua mwafaka zitachukuliwa baada ya ukaguzi wa ndani kukamilika.

Image: SCREENSHOT/ HISANI

Huduma ya polisi nchini (NPS) imelaani vikali tabia na matamshi ya makurutu wa GSU ambao walijirekodi na klipu yao kusambaa kote mitandaoni.

Kupitia kwa taarifa iliyotolewa Alhamisi jioni, NPS  imesema tabia ya makurutu hao kama ilivyoashiriwa kwenye video inayoenezwa mitandaoni haikubaliki na haiambatani na maadili ya kitengo cha GSU wala polisi kwa ujumla.

NPS imesema makurutu wote walipitia mafunzo muhimu kuhusiana na kanuni za kidemokrasia za polisi kwa lengo la kuwafanya maafisa wasikivu na wanaowajibika katika kazi yao ya kuhudumia umma. Huduma ya polisi imesema matamshi yaliyotolewa na  makurutu hao yanasikititisha sana.

"Tungependa kufafanua na kuwahakikishia umma kwamba tabia iliyoonyeshwa kwenye klipu hiyo haikubaliki na haiakisi maadili ya GSU, Huduma ya Polisi ya Kenya na Huduma ya Kitaifa ya Polisi. Wahitimu wote walipitia mafunzo makali yenye msingi wa thamani yaliyoigwa kwa kanuni za kidemokrasia za polisi na yaliyoundwa ili kuwafanya maafisa wa sheria wasikivu na wanaowajibika katika huduma ya raia.

Kiapo cha utiifu  walichokula wakati wa kuhitimu kwao ni kielelezo cha utakatifu wa wajibu wao wa utumishi. Kwa hivyo, matamshi kama yalivyotolewa kwenye klipu yanasikitisha na yamelaaniwa." Taarifa ya polisi ilisoma.

NPS imetoa hakikisho kwamba uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo unaendelea na hatua mwafaka zitachukuliwa baada ya ukaguzi wa ndani kukamilika.

"GSU inasifika kwa mafunzo yake mahususi yanayolenga kuzalisha maafisa wenye nidhamu na kuwajibika" NPS ilisema.

Katika video inayoenea mitandaoni, kikundi kidogo cha makurutu wa GSU  wenye umri wa ujana kinaoneka kuchangamka wanaposherehekea kukamilisha mafunzo yao.

Maafisa hao wanaonekana wakisakata densi  za kisasa kusherehekea kufuzu kwao huku wakijigamba kuhusu ukali wao wanapojiandaa kuanza kuhudumia taifa.

"Ndio hiyo, tiushamaliza.. mabang'a. Tunawakilisha, hii ni red barret.. tunakuja nje. Apana tambua. Hawa ni wale wazii, wabaya. Pa! Pa! Pa!" Maafisa hao wangesikika wakisema.

Wakenya ikiwemo viongozi wameendelea kutoa hisia tofauti kuhusiana na video hiyo baadhi yao  wakipendekeza adhabu kwa maafisa husika huku wengine wakiwatetea.