Jengo la gorofa 4 laporomoka Murang'a, wafanyakazi wanane wanaswa ndani

Muhtasari

•Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Murang'a, Donatha Kiplagat, alisema kwa bahati wafanyakazi wengi walikuwa wameenda kula chakula cha mchana wakati hayo yalitokea.

•Mkazi wa eneo hilo, Anthony Murimi, alisema wakati wa chakula cha mchana, walisikia kishindo na walipokimbilia eneo la tukio, walipata jengo hilo limeporomoka.

Jengo la ghorofa 4 lililoporomoka Murang'a Ijumaa Desemba 17, 2021
Jengo la ghorofa 4 lililoporomoka Murang'a Ijumaa Desemba 17, 2021
Image: BERNARD MUNYAO

Jengo la ghorofa nne lililokuwa linaendelea kujengwa liliporomoka  siku ya Ijumaa, na kuwanasa wafanyakazi wanane ndani.

Jengo hilo la hoteli ya Sun Star iliyoko karibu na mji wa Thika liliporomoka mwendo wa saa nane alasiri.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Murang'a, Donatha Kiplagat, alisema kwa bahati wafanyakazi wengi walikuwa wameenda kula chakula cha mchana wakati hayo yalitokea.

Alibaini kuwa wafanyikazi wawili waliondolewa kutoka kwa mabaki ya jengo wakiwa hai na kupelekwa katika Hospitali ya Thika Level 5.

Kamanda aliongeza kuwa jumla ya wafanyakazi 58 walikuwa wanafanya kazi katika pale lakini kwa bahati nzuri wengi walikuwa nje wakati nyumba hiyo ilipoanguka.

"Tumekusanya vifaa vya kusaidia katika zoezi la uokoaji. Kwa sasa, mchimbaji mmoja yuko ardhini tunaposubiri vifaa zaidi," alisema.

Kiplagat aliongeza kuwa wafanyakazi wote wa hoteli iliyo karibu wako salama, akisema walionasa katika jengo lililoporomoka ni wale wanaofanya kazi ya kuweka mabomba.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Majanga, Dkt Duncan Ochieng alisema wameomba vifaa na usaidizi kutoka kwa NYS na KDF kusaidia katika zoezi la uokoaji.

"Zoezi la uokoaji litaendelea usiku kucha na kufikia kesho tunatumai tutakuwa tumemaliza kazi ya uokoaji na uokoaji," aliongeza Ochieng.

Mkazi wa eneo hilo, Anthony Murimi, alisema wakati wa chakula cha mchana, walisikia kishindo na walipokimbilia eneo la tukio, walipata jengo hilo limeporomoka.

Matukio ya kuporomoka kwa nyumba nchini yameongezeka katika siku za hivi karibuni, na kuibua maswali juu ya viwango vya majengo yanayojengwa.

(Utafsiri: Samuel Maina)