Ataenda lini?Murkomen auliza baada ya Raila kuagizwa kufika mbele ya NCIC

Muhtasari
  • Maoni ya Murkomen yalikuja muda mfupi baada ya NCIC kutoa taarifa ikisema wamemwita Raila

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen sasa anataka DCI kumkamata mara moja kiongozi wa ODM Raila Odinga na kumweka korokoroni kufuatia matamshi ya 'madoadoa' aliyotoa Alhamisi huko Wajir.

Akijibu mwito wa NCIC, Seneta huyo aliibua maswali jinsi kesi ya kiongozi huyo wa ODM inavyoshughulikiwa.

Murkomen katika ujumbe wake wa Twitter alionekana kupendekeza Raila achukuliwe sawa na Seneta wa Meru Mithika Linturi ambaye alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa matamshi yake ya 'madoadoa' aliyotoa mjini Eldoret, Uasin Gishu.

"Mwanzo mzuri. Anaonekana lini? Je, ni siku atakayochagua? Kwako, ODPP inafanya kama ulivyomfanyia Mhe. Linturi na kwa DCI wako wapi Subarus? Tunatazama,” Murkomen alisema.

Maoni ya Murkomen yalikuja muda mfupi baada ya NCIC kutoa taarifa ikisema wamemwita Raila.

Wito huo ni kutafuta majibu kuhusu muktadha wa matamshi ya Raila 'madoadoa'.

"Tume inapenda kuwahakikishia Wakenya kujitolea kwake kuzuia aina yoyote ya matamshi ya chuki ili kuhakikisha Kenya inasalia kuwa taifa dhabiti, lenye ustawi na mshikamano na kutimiza ahadi yetu ya 'uchaguzi bila noma'," taarifa ya NCIC ilisema.

Siku ya Ijumaa kanara huyo wa ODM akiwa kaunti ya Kisumu wakati wa mkutano wa Azimo la Umoja aliomba msamaha kutokana na matamhi yake.