Wezi wawili wajipata taabani baada ya kujaribu kumwibia polisi Kiambu

Muhtasari

•Mwendesha bodaboda na abiria wake walimgeukia Mungai na kumshambulia kwa ngumi na mateke huku wakimwagiza awapatie pesa na vitu vingine vya thamani.

•Washukiwa walijaribu kutoroka ila Mungai akapiga gurudumu la pikipiki yao risasi na hapo wakalazimika kutii amri.

Crime Scene

Polisi katika kaunti ya Kiambu wanawazuilia washukiwa wawili wa wizi ambao walijaribu kumuibia afisa mmoja aliyevalia kiraia.

Koplo Nahashon Mungai ambaye anafanya kazi katika kituo cha polisi cha Kiambu alikuwa ameabiri bodaboda ili kupelekwa hadi kijiji cha GG, eneo la Thindigua wakati tukio hilo lilitokea.

Wakiwa njiani, mwendesha bodaboda alichukua abiria mwingine ambaye walishirikiana naye kumgeukia Mungai na kumshambulia kwa ngumi na mateke huku wakimwagiza awapatie pesa na vitu vingine vya thamani.

Katika harakati zile afisa yule alitoa bastola yake ambayo alikuwa amefunga kiunoni na kuwaamuru wajisalimishe. Washukiwa kuona vile walijaribu kutoroka ila Mungai akapiga gurudumu la pikipiki yao risasi na hapo wakalazimika kutii amri.

Mhasiriwa aliwakamata wawili hao na kuwaita polisi wenzake kutoka kituo cha Thindigua ambao wakiwapeleka kizuizini.

Kitengo cha DCI kimemsherehekea koplo Mungai kwa ujasiri na ushujaa ambao alionyesha wakati wa tukio hilo.