Watu 6 wauawa, 8 wajeruhiwa katika mashambulizi ya kijambazi Isiolo

Muhtasari

•Majambazi waliwaua watu watatu wa familia moja; mama, watoto wawili wenye umri wa miaka mitatu na 10 na kumjeruhi baba yao.

•Waliojeruhiwa wamelazwa katika kituo cha afya cha Merti huku wengine wakipewa rufaa hadi hospitali kuu ya Isiolo wakiwa na majeraha mabaya ya risasi.

Crime Scene

Watu sita waliuawa na wengine wanane kujeruhiwa katika eneo la Degogicha kaunti ya Isiolo baada ya majambazi waliokuwa wamejihami vikali kuvamia kijiji kimoja na kutoroka na idadi isiyojulikana ya mifugo.

Majambazi hao walishambulia Jumamosi alfajiri na kuua watu watatu wa familia moja; mama, watoto wawili wenye umri wa miaka mitatu na kumi na kumjeruhi baba.

Waliwauwa watu wengine watatu na kuwajeruhi wengine saba katika vita vikali vya risasi na wakaazi vilivyodumu kwa saa kadhaa huku wakiwaiba mifugo hao.

Kamishna wa Kaunti ya Isiolo, Geoffrey Omonding alithibitisha kisa hicho akisema kikosi cha maafisa wa polisi kimetumwa kuwasaka watu wanaoshukiwa kuwa wavamizi.

Alisema waliojeruhiwa wamelazwa katika kituo cha afya cha Merti huku wengine wakipewa rufaa hadi hospitali kuu ya Isiolo wakiwa na majeraha mabaya ya risasi.

Mgombea kiti cha ugavana wa Isiolo Abdi Guyo alitaja kisa hicho kuwa cha kusikitisha na kutoa wito kwa vyombo vya usalama kufanya hara ili kuzuia mauaji zaidi.

Mnamo Machi, watu watano waliuawa kufuatia mapigano kati ya jamii mbili za wafugaji katika eneo la Degogicha.

Mnamo Juni 10, wafugaji watatu na wengine saba walijeruhiwa vibaya katika shambulio la kijambazi la alfajiri huko Chinchoftu katika wadi ya Cherab kaunti ya Isiolo.

Guyo alisikitika kuwa kaunti hiyo inakabiliwa na maswala mazito ya kiusalama na akataka kutumwa kwa askari zaidi wa polisi wa akiba ili kuzuia washambuliaji kutoka kaunti jirani.

"Tulipoteza maisha zaidi ya kumi na wengine 13 wanauguza majeraha ya risasi kutokana na mauaji ya kiholela na mashambulizi ya ujambazi katika muda wa wiki moja" Guyo alisema.