DPP Haji aagiza EACC kuchunguza uhamisho wa wapiga kura Wajir, Garissa

Uhamisho unaodaiwa ni kinyume na kifungu cha 3 na 6 cha Sheria ya Makosa ya Uchaguzi, 2016.

Muhtasari
  • DPP Haji aagiza EACC kuchunguza uhamisho wa wapiga kura Wajir, Garissa
Picha ya makao makuu ya EACC jijini Nairobi
Picha ya makao makuu ya EACC jijini Nairobi
Image: MAKTABA

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji ameagiza Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi kuchunguza madai ya uhamisho wa wapigakura kinyume cha sheria huko Wajir na Garissa.

Haya ni kwa mujibu wa barua iliyoandikwa Alhamisi, Agosti 4, na Haji kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak.

"Ninaagiza kwamba ufanye uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma hizo na kisha uwasilishe faili la uchunguzi wa matokeo ili lipitiwe na maelekezo zaidi," inasomeka barua hiyo.

Uhamisho unaodaiwa ni kinyume na kifungu cha 3 na 6 cha Sheria ya Makosa ya Uchaguzi, 2016.

Haji alisema alipokea barua ya kusambaza Ripoti ya Uchunguzi wa Awali kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein ikisema wapiga kura kutoka Eldas huko Wajir na Balambala huko Garissa walikuwa wakihamishwa isivyo kawaida.

PIR ilionyesha kuwa wafanyikazi watano katika bodi ya uchaguzi walihusika.

Wao ni pamoja na; Afisa wa ICT wa IEBC Garissa Adan Salah, ambaye ni afisa wa zamani wa ICT katika Wajir, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ijara na aliyekuwa RO Eldas Issack Muhumed na RO Wajir Kaskazini Abdulahi Musa Mohammed, ambaye pia ni aliyekuwa RO Balambala.

Wengine waliohusika ni, aliyekuwa naibu RO Balambala Mohammed Maow Abdi na RO Balambala Ali Noor Hussein.

Mnamo Jumatano, ripoti mpya ya Ukaguzi ya KPMG ilionyesha kuwa watu wasioidhinishwa walipata hifadhidata ya sajili ya wapigakura ya IEBC.

Ilisema watumiaji ambao hawajaidhinishwa walisasisha rejista ya wapiga kura.

"Njia za ukaguzi zilionyesha kuwa kulikuwa na watumiaji ambao hawakutangazwa kwenye gazeti la serikali kama wasimamizi wa uchaguzi au wasimamizi wasaidizi waliosasisha data ya wapiga kura," ripoti ya KPMG ilisoma.

IEBC, hata hivyo, ilikanusha kuwa watu wasiowafahamu walifikia mfumo huo, ikisema uchunguzi wake ulibaini kuwa watumiaji hao waliidhinishwa vilivyo.

"Uchunguzi ulifanywa na matokeo yalionyesha kuwa shughuli za kusasisha wapigakura zilifanywa na maafisa wa usajili walioidhinishwa ipasavyo," IEBC ilisema katika majibu yake kwa swali la KPMG.