Familia ya Embu yalilia haki baada ya jamaa kuuawa na gari la polisi

Walioshuhudia walisema gari hilo la polisi lilimgonga kaka yake na kuondoka kwa kasi.

Muhtasari

•Daniel Murithi, 44, alikumbana na kifo chake baada ya pikipiki yake kugongana na gari la polisi huko Kirigi kando ya barabara ya Manyatta-Kianjokoma Jumanne jioni.

•Nduguye marehemu alisema polisi katika kituo cha polisi cha Ngimari huko Manyatta waliwazungusha miduara walipohoji kuhusu uchunguzi.

Mkewe Daniel Murithi Wincate Mukami akiomboleza kifo cha mumewe aliyefariki baada ya pikipiki yake kugongana na gari la polisi mnamo Jumanne, Agosti 16.
Mkewe Daniel Murithi Wincate Mukami akiomboleza kifo cha mumewe aliyefariki baada ya pikipiki yake kugongana na gari la polisi mnamo Jumanne, Agosti 16.
Image: BENJAMIN NYAGA

Familia moja eneo la Mbuinjeru, Embu Mashariki inalilia haki baada ya mmoja wao kufariki kwenye ajali inayodaiwa kusababishwa na gari la polisi aina ya toyota landcruiser.

Daniel Murithi, 44, alikumbana na kifo chake baada ya pikipiki yake kugongana na gari la polisi huko Kirigi kando ya barabara ya Manyatta-Kianjokoma Jumanne jioni.

Kakake Murithi, Moses Nyaga Kamunti alisema walioshuhudia walisema gari la polisi wanaofanya kazi katika kaunti ndogo ya Embu Kaskazini lilimgonga kaka yake na kuondoka kwa kasi. Kamunti alizungumza Ijumaa nyumbani kwao Mbuinjeru.

“Ndugu yangu aligongwa na gari la polisi likaondoka kwa kasi, hawakujishughulisha hata kumkimbiza hospitali, labda maisha ya kaka yangu yangeweza kuokolewa,” alisema.

Kamunti alisema kaka yake aliachwa kama amelala kando ya barabara kwa uchungu hadi watu wema walipomkimbiza katika Hospitali ya Embu Level 5 umbali wa kilomita 10 hivi.

“Alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu, muda mfupi baada ya kuwasili,” alisema.

MAREHEMU: Daniel Murithi aliyefariki baada ya pikipiki yake kugongana na gari la polisi eneo la Kirigi huko Manyatta mnamo Jumanne, Agosti 16.
MAREHEMU: Daniel Murithi aliyefariki baada ya pikipiki yake kugongana na gari la polisi eneo la Kirigi huko Manyatta mnamo Jumanne, Agosti 16.
Image: BENJAMIN NYAGA

Familia iliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Ngimari, ambacho ni kituo cha karibu zaidi na eneo la ajali lakini maafisa hao wakawaambia gari la polisi na pikipiki ya marehemu ilikuwa imechukuliwa na kamanda wa trafiki wa Embu Magharibi.

Kamunti alisema polisi katika kituo cha polisi cha Ngimari huko Manyatta waliwazungusha miduara walipohoji kuhusu uchunguzi.

“Siku ya Alhamisi, tulikwenda kituoni kuandikisha maelezo yetu na kukuta askari aliyedaiwa kusababisha ajali hiyo, alikuwa tayari ameandika taarifa  yake lakini tulinyimwa maelezo  yake.

“Tulitakiwa kurejea baadaye na kuwasilisha leseni ya udereva ya marehemu, kitambulisho, bima ya pikipiki iliyokuwa kwenye pikipiki na fedha taslimu kwa ajili ya uchunguzi wa maiti,” alisema.

Alisema Murithi aliondoka nyumbani kuelekea Embu mjini, kununua gurudumu la tuk-tuk kwa vile alitegemea sana gari hilo kwa biashara ya usafiri.

Mukami alisema Murithi aliondoka nyumbani mwendo wa saa kumi jioni na hakurejea.

“Niliwahi kumuuliza kwa nini anachelewa kusafiri lakini akaniambia alikuwa amezungumza na mfanyabiashara huyo ambaye alimwambia angefunga saa moja usiku.

"Alisema kuna muda wa kutosha wa kwenda na kurudi nyumbani, ambapo hakurudi tena," alisema.

Familia hiyo inataka haki itendeke kwa Daniel Murithi anayetoka Mbogori eneo la Mbuinjeru, takriban kilomita tatu kutoka Kianjokoma.

Haya yanajiri huku ndugu wawili kutoka Kianjokoma wakidaiwa kufariki mikononi mwa polisi, mwaka mmoja uliopita.

 Naibu kamishna wa kaunti ya Embu Kaskazini William Owino alisema kuwa dereva anayedaiwa kusababisha ajali hiyo aliepuka shambulio kutoka kwa wakazi lakini akaendelea na kuripoti kwa polisi.

"Eneo hilo halikuwa na matuta na dereva alikwepa shambulio kutoka kwa umati wa watu wenye hasira. Hata hivyo, alikimbilia kituo cha polisi kilicho karibu na kuripoti tukio hilo," alisema.

Kamishna huyo alisema kesi iko polisi na mchakato wa kuhudumia familia kwa haki inayostahiki unaendelea.

Murithi ameacha mke na watoto wawili wenye huzuni, mwenye umri wa miaka 15 ambaye yuko kidato cha kwanza na mtoto wa miaka mitatu ambaye angejiunga na shule muhula ujao, ambao wote walikuwa wakimtegemea.