Mwanamume auawa, sehemu za siri zakatwa na mwili kuning'inizwa kwenye mti Murang'a

Kulikuwa na visu na panga vilivyoachwa katika eneo la tukio.

Muhtasari

•Mwili wa Charles Moko ulipatikana na kakake Simon Mburu shambani na alikuwa amevuliwa nguo.

•"Mwili wake ulikuwa na majeraha ya visu kifuani na sehemu zake za siri zilikuwa zimekatwa na kuachwa karibu na mwili," Mburu alisema.

crime scene
crime scene

Kijiji cha Kari katika kaunti ndogo ya Kahuro, Kaunti ya Murang’a kilikumbwa na Mshtuko baada ya mwili wa mwanamume mwenye umri wa miaka 31 kupatikana ukining’inia juu ya mti siku ya Ijumaa.

Mwili wa Charles Moko ulipatikana na kakake Simon Mburu shambani na alikuwa amevuliwa nguo.

Mburu alisema aliona kitu kikining’inia kwenye mti na akasogea karibu ndipo akagundua ni nduguye aliyeuawa.

"Mwili wake ulikuwa na majeraha ya visu kifuani na sehemu zake za siri zilikuwa zimekatwa na kuachwa karibu na mwili," Mburu alisema.

Alithibitisha kuwa kulikuwa na visu na panga vilivyoachwa katika eneo la tukio na vitu vingine ambavyo marehemu alitumia katika kazi yake kwenye bucha katika kituo cha biashara cha Kari.

Mary Waithera, jirani yake alisema mauaji hayo yameacha kijiji katika hali tete na kwamba hawawezi kuelewa ni kwa nini mtu yeyote angefanya kitendo hicho cha kinyama.

Alisema Moko alikuwa mwanamume mchapakazi na kwamba alikuwa ameajiriwa kuchoma nyama katika bucha.

Lakini baadhi ya wenyeji walisema tabia yake ilikuwa ya kutiliwa shaka na kwamba alikamatwa mara kwa mara baada ya kupatikana na bangi.

“Pia alikuwa mkaidi sana. Hukuweza kumpeleka popote. Nilimwambia akome kuvuta bangi mara nyingi lakini hakunisikiliza,” jamaa alisema.

Naibu kamishna wa kaunti ya Kahuro Fred Muli alithibitisha kuwa marehemu alikatwa viungo vyake vya siri.