Polisi amfyatulia risasi mkewe kabla ya kujigeuzia bunduki na kujiua Bondo

Mkewe Kyalo, ambaye alipigwa risasi kwenye matako, kwa sasa anauguza majeraha katika Hospitali

Muhtasari

•Polisi walisema marehemu kwanza alimpiga risasi na kumjeruhi mke kabla ya kujiguezia bunduki.

•Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, polisi walisema wakihusisha ufyatuaji risasi huo na msongo wa mawazo kazini.

Bunduki
Bunduki
Image: Andrew Kasuku

Polisi mmoja alifariki kwa kujitoa uhai muda mfupi baada ya kumpiga risasi na kumjeruhi mkewe katika Kituo cha Polisi cha Bondo katika Kaunti ya Siaya.

Polisi walisema marehemu kwanza alimpiga risasi na kumjeruhi mke kabla ya kujiguezia bunduki.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Bondo Ibrahim Kosi alisema afisa huyo aliyefariki, Michael Kyalo, aliripoti kazini kama kawaida Ijumaa Julai 7 ambapo alipewa bunduki.

Hata hivyo, badala ya kuelekea kwenye kituo cha kazi alichopangiwa, Kyalo alitembea hadi nyumbani kwake ambapo kisa hicho kilitokea Jumamosi asubuhi.

Mkewe Kyalo, ambaye alipigwa risasi kwenye matako, kwa sasa anauguza majeraha katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Bondo huku mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha kituo hicho cha afya.

Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, polisi walisema wakihusisha ufyatuaji risasi huo na msongo wa mawazo kazini.

Kesi kama hizo zinahusishwa na shinikiz la kijamii ambalo limesababisha matukio mengi ya mauaji na kujiua, polisi walisema.

Hadi visa vitatu vya kujitoa uhai vinaripotiwa kila siku nchini kwa kasi ya kutisha.

Visa vya watu kujiua vimeongezeka mwaka huu na viongozi wanalaumu hali hiyo kuwa ni msongo wa mawazo.

Polisi walishughulikia kesi 499 mnamo 2019, na 575 mnamo 2020.

Takriban watu 313 wameripotiwa kujiua kati ya Januari na Julai 2021.

Wengi wa wahasiriwa walikuwa wanaume, ripoti za polisi zinasema.

Kuna msukumo wa kushughulikia tishio.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema visa hivyo vinachangiwa na ukosefu wa ajira, kuvunjika kwa mahusiano au kifo, kushindwa kitaaluma au shinikizo.

Nyingine ni pamoja na matatizo ya kisheria, matatizo ya kifedha, uonevu, majaribio ya awali ya kujiua, historia ya kujiua katika familia, ulevi na matumizi mabaya ya vileo, mfadhaiko na ugonjwa wa msongo wa mawazo.

Ulimwenguni kote, karibu watu 800,000 hufa kwa kujiua kila mwaka huku takriban asilimia 78 ya visa vikitokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.