Babake Kiptum asema bado ana uchungu wiki kadhaa baada ya kifo cha mwanawe

Babake Kelvin Kiptum amekiri bado ana uchungu kwa zaidi ya mwezi mmoja baada ya kumpoteza mwanawe katika ajali ya barabarani.

Muhtasari
  • Alisema iwapo kutakuwa na mchezo mchafu atasalimisha suala hilo kwa Mungu, kwani yeye ni mzazi ambaye anaumwa sana.
Mwanapatholojia mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor akizungumza katika chumba cha maiti cha hospitali ya Eldoret. 21/02/2024.
Mwanapatholojia mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor akizungumza katika chumba cha maiti cha hospitali ya Eldoret. 21/02/2024.
Image: MATHEWS NDANYI

Babake Kelvin Kiptum amekiri bado ana uchungu zaidi ya mwezi mmoja baada ya kumpoteza mwanawe katika ajali ya barabarani.

Kiptum mwanariadha mashuhuri wa mbio za marathoni, alifariki Februari 2024 pamoja na kocha wake baada ya gari alilokuwa akiendesha  kupata ajali.

Jumatano Machi 20, babake Kiptum alisema yuko tayari kuendelea na maisha yake endapo tu kifo cha mwanawe itabainika kuwa ilikuwa ajali ya asili bila mchezo mchafu.

Alisema iwapo kutakuwa na mchezo mchafu atasalimisha suala hilo kwa Mungu, kwani yeye ni mzazi ambaye anaumwa sana.

"Ikiwa kungekuwa na mtu ambaye alihusika katika kifo cha mwanangu, ningemwachia Mungu suala hilo. Nasema hivi kama mzazi mwenye maumivu makali sana. Ninajua pia kuwa ajali hutokea kila wakati, kwa hivyo ikiwa ni ajali tu, nitakubali", alisema.

Alizungumza baada ya kukutana na katibu wa baraza la mawaziri la michezo Ababu Namwamba wakati wa kutambulisha mwanariadha aliyekufa katika ukumbi wa "Talanta of Fame."

Waziri aliihakikishia familia ya marehemu Kiptum msaada wa serikali kwao.

Huku akitambua mafanikio ya Kiptum katika maisha yake, Waziri huyo alisema serikali ina nia ya kukuza talanta zaidi kutoka eneo hilo.

Waziri huyo aliungana na familia ya marehemu aliyefariki ikiongozwa na babake Cheruiyot, mama Kangogo na mkewe Asenath na watoto wao wawili.