Wafanyikazi 2 wakuu wa bunge la kaunti ya Kisumu waaga dunia

Muhtasari
  • Wafanyikazi wawili wakuu wa bunge la kaunti ya Kisumu waaga dunia
  • Wawili hao walifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi kulingana na uongozi wa bunge la kaunti hiyo
Lazarus Obera na Nelco Sagwe

HABARI NA FAITH MATETE;

Bunge la kaunti ya Kisumu limepoteza wafanyikazi wake wawili wakuu, naibu Karani Nelco Sagwe na msimamizi Mwandamizi wa Rasilimali Watu Askofu Mkuu Lazarus Obera.

Wawili hao walifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi kulingana na uongozi wa bunge la kaunti hiyo.

Kulingana na taarifa ya Spika wa Bunge Elisha Oraro na Karani Owen Ojuok, wawili hao walikuwa wafanyikazi wa kujitolea na wenye nidhamu ambao uongozi wao wa mabadiliko utakosekana na Bunge na haswa wafanyikazi waliowashauri.

"Sagwe, mwanafunzi aliye hitimu shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alikuwa mfanyikazi wa serikali mwenye uzoefu mkubwa, aliyejitolea na mwenye nidhamu", walisema.

Walisema bunge hilo limepoteza mfanyikazi aliyejitolea, mwenye bidii na wa kidini (Obera) - mzee ambaye alikuwa chanzo cha msukumo kwa watu wengi na ambaye alikuwa na jukumu la mshauri na mpatanishi katika Bunge hilo.

"Kwa niaba ya Wajumbe wa Bunge la Kaunti ya Kisumu, uongozi wa Bunge na wafanyikazi, tunapenda kutoa rambirambi zetu za dhati kwa familia na marafiki wa marehemu".

Vifo vya wawili hao vinajiri baada ya kaunti hiyo kuwa machoni mwa serikali baada ya miezi michache iliyopita kurekodi aina mpya ya virusi vya corona.

Ni jambo ambalo lilimlazimu rais kuweka vikwazo vipya katika kaunti kumi na tatu Kisumu ikiwa miongoni mwa kaunti hizo, ili kuthibiti kuenea kwa maambukizi hayo.