Tahadhari yatolewa kuhusu tishio la shambulizi la kigaidi Kenya

Muhtasari

• Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa iliwatahadharisha raia wake kuepuka maeneo ya umma na maeneo yenye msongamano wa watu ambazo ndizo sehemu zinazolengwa kwa mashambulizi.

• Maeneo hayo ni hoteli, mikahawa, maeneo ya burudani na vituo vya kibiashara jijini.

• Ubalozi wa Ujerumani pia ulitoa onyo.

Mafisa wa polisi wakishika doria katika eneo la Lamu
Mafisa wa polisi wakishika doria katika eneo la Lamu
Image: MAKTABA

Vitengo vya usalama vimeimarisha operesheni ili kusambaratisha mipango yoyote ya ugaidi nchini Kenya.

Polisi hata hivyo wamewataka wananchi kuendelea kuwa waangalifu na kuonya kuwa kutakuwa na oparesheni za kiusalama ambazo huenda zitaathiri shughuli za kawaida katika baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na barabara kuu na majengo.

Hii ni baada ya serikali ya Ufaransa kutoa tahadhari kwa raia wake nchini Kenya kuhusu uwezekano wa shambulizi la kigaidi jijini Nairobi na ambalo linalenga maeneo yanayotembelewa na wageni.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa iliwatahadharisha raia wake pamoja na wahamiaji kutoka nchi nyingine za Magharibi kuepuka maeneo ya umma na maeneo yenye msongamano wa watu ambazo ndizo sehemu zinazolengwa kwa mashambulizi.

Maeneo hayo ni hoteli, mikahawa, maeneo ya burudani na vituo vya kibiashara jijini.

Ilitoa wito kwa wageni wanaoishi na kufanya kazi jijini Nairobi kuwa waangalifu sana katika siku zijazo, haswa wikendi hii.

Ubalozi wa Ujerumani pia ulitoa onyo kwamba katika siku chache zijazo raia wake nchini Kenya wanapaswa kuwa makini zaidi wanapokuwa katika maeneo ya umma.

Ubalozi huo umetaka raia wake kufuata kanuni na miongozo ya kiusalama.