Mbunge afariki baada ya kugongwa na bodaboda South B, Nairobi

Mbunge huyo alifariki katika kituo cha afya alikokuwa akipata matibabu kutokana na majeraha ya kichwa.

Muhtasari

• Mbunge huyo aligongwa na pikipiki na kupata majeraha ya kichwa.

• Mbunge huyo atazikwa mwendo wa saa kumi jioni ya leo Jumatano katika makaburi ya waislamu eneo la Lang’ata jijini Nairobi.

Kulow Maalim, Banisa MP
Kulow Maalim, Banisa MP
Image: Twitter

Mbunge wa Banissa, Kulow Hassan Maalim amefariki dunia baada ya kugongwa na bodaboda siku ya Jumapili katika mtaa wa South B jijini Nairobi.

Kulingana na ripoti kutoka kwa familia yake, Mbunge huyo kutoka kaunti ya Garissa alifariki mapema alfajiri ya Jumatano katika kituo kimoja cha afya alikokuwa akipata matibabu.

Mbunge huyo aligongwa na pikipiki na kupata majeraha ya kichwa.

Mbunge huyo atazikwa mwendo wa saa kumi jioni ya leo Jumatano katika makaburi ya waislamu eneo la Lang’ata jijini Nairobi.

Marehemu mbunge amewakilisha eneo bunge la Banissa katika Bunge la Agosti tangu 2017. Pia aliwahi kuwa mwanachama wa Kamati ya Idara ya Uchukuzi, Kazi za Umma na Makazi.

Wenzake, wakiongozwa na mbunge wa Eldas Adan Keynan wamemwomboleza kama kiongozi mashuhuri na mtumishi wa umma aliyejitolea.

"Kulow alikuwa kielelezo cha kiongozi mashuhuri, mtumishi wa umma aliyejitolea na mtu anayependeza katika jamii ambaye alitekeleza majukumu yake ya uongozi kwa heshima na ustadi mkubwa," Keynan alisema.Mbunge wa Mandera Magharibi Adan Haji Yussuf Adan Haji alituma salamu za rambirambi kwa wananchi wa Banissa na familia ya marehemu mwenzake.

"Maalim alikuwa kiongozi mkuu na Muislamu aliyejitolea ambaye amekuwa na nafasi muhimu katika jamii yetu," alisema.