Yesu wa Tongaren kukaa rumande siku 4 zaidi, kufanyiwa uchunguzi wa kiakili

Upande wa mashtaka ulikuwa umeomba muda wa siku saba kwa uchunguzi kamili kuhusu mafundisho na shughuli za Wekesa.

Muhtasari

• Kesi hiyo itatajwa Mei 16.

• Mhubiri huyo mwenye utata mapema Jumatatu alidai kwamba hafanyi lolote isipokuwa kuhubiri injili ya kweli.

Yesu wa Tongaren kufanyiwa uchunguzi wa akili.
Yesu wa Tongaren kufanyiwa uchunguzi wa akili.
Image: Maktaba

Eliud Wekesa, anayejiita ‘Yesu wa Tongaren’ atasalia kwa siku nne zaidi chini ya ulinzi wa polisi, mahakama ya Bungoma imeamuru.

Wekesa aliwasilishwa mahakamani siku ya Ijumaa ambapo makachero wa polisi walitafuta siku zaidi kukamilisha uchunguzi kuhusu mhubiri huyo.

Hakimu Mkuu Mfawidhi, Tom Mark Olando alisema kipindi hicho ni kuwezesha polisi kumchukua mshtakiwa kwa uchunguzi wa kiakili na kufanya upekuzi katika kanisa na maeneo ya mtuhumiwa.

Kesi hiyo itatajwa Mei 16.

Upande wa mashtaka ulikuwa umeomba muda wa siku saba kwa uchunguzi kamili kuhusu mafundisho na shughuli za Wekesa.

Katika hati yake ya kiapo, upande wa mashtaka ulidai kanisa la Wekesa, New Jerusalem, halijasajiliwa kisheria.

Wekesa alijiwasilisha kwa polisi kwa hiari Jumatano kufuatia wito wa kuhojiwa kuhusu mafundisho na shughuli zake za kidini.

Huku akiwa ameandamana na wafuasi wake, Wekesa aliomba asikamatwe, akieleza kuwa hana la kuficha. Hata hivyo, polisi walisisitiza kumshikilia kwa mahojiano zaidi ili kuongoza hatua inayofuata.

Mhubiri huyo mwenye utata mapema Jumatatu alidai kwamba hafanyi lolote isipokuwa kuhubiri injili ya kweli.