Hukumu

Kiongozi wa waasi DR Congo afungwa maisha kwa kutekeleza uhalifu dhidi ya binadamu

Mahakama ya kijeshi ilimpata Ntabo Ntaberi na hatia ya mauaji, ubakaji, na utumwa wa kingono

Muhtasari

 

  • Uamuzi huo ulitolewa baada ya kusikilizwa kwa kesi hiyo iliochukua takriban miaka miwili ambapo waathiriwa 178 walitoa ushahidi wao.
  • Eneo la mashariki mwa DRC limezongwa na mizozo , iliochochewa na migawanyiko ya kisiasa mbali na utajiri wa raslimali katika eneo hilo.
Ntabo Ntaberi

Na BBC 

Aliyekuwa kiongozi wa wanamgambo katika taifa la jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo ubakaji wa watu wengi.

Mahakama ya kijeshi ilimpata Ntabo Ntaberi na hatia ya mauaji, ubakaji, utumwa wa kingono na kuwasajili watoto walio chini ya miaka 15 katika jeshi lake.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya kusikilizwa kwa kesi hiyo iliochukua takriban miaka miwili ambapo waathiriwa 178 walitoa ushahidi wao.

 

Umoja wa Mataifa unasema kwamba umauzi huo umeonesha 'uzoefu wa kutenda uhalifu bila kujali una kikomo chake'.

'Uamuzi huo unawapatia matumaini waathiriwa wa mzozo huo wa DRC , mateso waliopitia yamesikilizwa na kutambuliwa', alisema Leila Zerrougui , mkuu wa ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa uliopo nchini DR Congo.

Ntaberi anayejulikana kama Sheka , alikuwa mmoja wa viongozi wa kundi moja la wapiganaji kwa jina Nduma of Congo{NDC} ambalo lilifanya operesheni zake katika mkoa wa mashariki wa Kivu.

Eneo la mashariki mwa DRC limezongwa na mizozo , iliochochewa na migawanyiko ya kisiasa mbali na utajiri wa raslimali katika eneo hilo.

Kulikuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini DR Congo kati ya 1998 na 2003, lakini baadhi ya wapiganaji wanendelea kupigana mbali na kusababisha mateso katika eneo hilo ambapo uujumbe wa UN unatatizika kuleta amani.

Mamlaka mara ya kwanza ilitoa agizo la kukamatwa kwa Ntaberi mnamo mwezi Januari 2011, ikimshutumu kwa kutekeleza uvamizi katika vijiji katikati ya mwaka 2010.

Wakati wa uvamizi huo , wapiganaji a kundi lake la NDC pamoja na makundi mengine mawili walidaiwa kuwabaka takriban watu 400 na kuwauwa wengine 300.

 

Ntaberi alikuwa mafichoni kwa takriban miaka sita , lakini hatimaye akasalimu amri na kujiwasilisha kwa Ujumbe wa amani wa Umoja wa mataifa nchini DR Congo 2017.

Alishatakiwa pamoja na wandani wake watatu , akiwemo kamanda mmoja kutoka kwa wapiganaji wengine ambaye pia alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kutekeleza uhalifu katika eneo la Kivu kaskazini.

Hukumu yao jela ilitolewa katika mahakama iliokuwa katika mji wa Goma siku ya Jumatatu.

''Tumeridhika na uamuzi uliotolewa , ni ishara kubwa kwa wababe wengine wa kivita '', alisema Kahindo Fatuma , msemaji anayewawakilisha waathiriwa akizungumza na chombo cha habari cha AFP .

Thomas Fessy, mtafiti kuhusu masuala ya haki za kibinadamu katika shirika la Human Rights Watch nchini DR Congo alisema kwamba hukumu dhidi ya Ntaberi ni hatua kubwa katika kukabiliana na utekelezaji wa uovu bila kujali

Makumi ya makundi yaliojihami yanaendelea kutekeleza uhalifu mashariki mwa DR Congo .

Tawi moja la wapiganaji wa Ntaberi bado linaendeleza operesheni zake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo chini ya jina NDC Renovated { NDC ilioimarika}