Mtu mmoja afariki baada ya wafuasi wa Trump kuvamia bunge

Muhtasari

  • Uchaguzi wa Marekani 2020: Mtu mmoja afariki baada ya wafuasi wa Trump kuvamia bunge.

  • Bado maafisa hawajataja jina la mwanamke huyo lakini polisi wanasema alikuwa raia wa kawaida.

Image: GETTY IMAGES

Polisi imethibitisha kuwa mwanamke mmoja aliyepigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea baada ya wafuasi wa Trump kuvamia bunge, amefariki dunia kwasababu ya majeraha aliyopata.

Bado maafisa hawajataja jina la mwanamke huyo lakini polisi wanasema alikuwa raia wa kawaida.

Aidha, mtu mwingine amepigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea ndani ya bunge la Marekani, kulingana na shirika la habari la Associated Press.

Lindsay Watts, mwanahabari wa shirika lenye kuhusishwa na Fox News, ameandika ujumbe kwenye Twitter kuwa wahudumu wa afya wa Washington DC walisema juhudi za kumuokoa mwanamke mmoja aliye kwenye hali mahututi zinaendelea baada ya kupigwa risasi kifuani.

Wafuasi wa Trump waliokuwa na hasira waliandamana huku wakiimba, "Tunamtaka Trump" huku mmoja wao akipigwa picha akiwa ameketi kwenye kiti cha rais wa bunge la Seneti.

Polisi Washington imesema kuwa ni wazi waandamanji hao walikuwa tayari kutumia nguvu yoyote ile kuingia katika majengo ya bunge.

Huku akiwa ameketi katika kiti cha spika wa bunge la wawakilishi Nancy Pelosi mmoja wa waandamanaji hao aliwacha ujumbe uliosema hatutakubali
Huku akiwa ameketi katika kiti cha spika wa bunge la wawakilishi Nancy Pelosi mmoja wa waandamanaji hao aliwacha ujumbe uliosema hatutakubali
Image: EPA

Inasemekana hadi kufikia sasa watu 13 na silaha tano zimenaswa na polisi wakati ghasia zinaendelea bungeni.

Maafisa polisi wa Washington DC wamesema wamepata bunduki tano ikiwemo za mkononi na ndefu.

Mkuu wa polisi Robert Contee amewaambia wanahabari kuwa waliokamatwa sio wakazi wa eneo la DC.

Vitoa machozi vilitumika kuwatawanya waandamanaji hao
Vitoa machozi vilitumika kuwatawanya waandamanaji hao
Image: REUTERS

Baada ya uvamizi huo uliochukua saa kadhaa, afisa anayesimamia mipangilio ya bungeni alitangaza kuwa sasa jengo hilo limenusuriwa na vikosi vya usalama.

Wakati mmoja Bwana Trump alilazimika kurekodi ujumbe kwenye video na kuutuma katika mtandao wa Twitter akitoa wito kwa wafuasi wake kuondoka katika majengo ya bunge lakini naye akawa anaendelea madai yasiokuwa na ushahidi wowote kuwa Democrats waliiba kura.

Lakini kukawa na ishara kidogo zinazoonesha kwamba waandamanaji hao wanatii wito wa Trump unaowataka warejee nyumbani licha ya kwamba mji huo wote unatekeleza hatua ya kutoka nje kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi kumi na mbili asubuhi.

"Najua machungu yenu, najua mumevunjika moyo," Trump alisema. "Lakini lazima sasa murejee nyumbani, lazima tuwe na amani ... hatutaki yeyote ajeruhiwe."

Bwana Biden kwa upande wake amesema maandamano hayo "yamesababishwa na uchochezi na ni lazima hilo likome sasa", amesema.

Wanajeshi na maafisa wa polisi pia wamepelekwa katika majimbo jirani huku maafisa wa shirika la ujasusi FBI wakipelekwa katika majengo ya bunge kusaidiana na maafisa wa polisi.

Mwandamanaji mmoja aruka kutoka juu na kuingia katika bunge la seneti
Mwandamanaji mmoja aruka kutoka juu na kuingia katika bunge la seneti
Image: GETTY IMAGES

Pia amethbitisha kuwa baadhi ya maafisa wanapata matibabu baada ya kujeruhiwa.

Wafuasi wa Donald Trump wenye hasira wamevuka mipaka ya usalama iliyowekwa na kusimama kandokando ya bunge huko Washington, wakati wabunge wanakutana kumuidhinisha rais mteule Joe Biden kama mshindi wa uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana.

Katika matukio ya kutatanisha, waandamanaji walizunguka jengo la bunge huku wabunge nao wakisindikizwa kutoka bungeni humo na polisi.

Bwana Biden alisema huo ni "uasi", huku Bwana Trump kwa upande wake akatoa ujumbe kwa njia ya video akiwataka wafuasi wake kutoka bungeni na kurejea nyumbani.

Maafisa wa polisi walikabiliana na wafuasi wao huku baadhi yao wakijeruhiwa
Maafisa wa polisi walikabiliana na wafuasi wao huku baadhi yao wakijeruhiwa
Image: REUTERS

Kikao cha pamoja cha bunge kuidhinisha ushindi wa Bwana Biden kimeahirishwa na bunge limelazimika kwenda mapumzikoni.

Kuna taarifa kuwa watu walitumia bunduki kwenye jengo hilo .Pia mabomu ya kutoa machozi yametumika kutawanya waandamanaji.