Othman Masoud ateuliwa kuwa makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar

Muhtasari
  • Othman Masoud ateuliwa kuwa mrithi wa Maalim Seif Sharif Hamad
  • Uteuzi wa Masoud umefanywa na Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi baada ya mashauriano na chama cha ACT-Wazalendo

Othman Masoud ateuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kuchukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki tarehe 17 Februari mwaka huu.

Uteuzi wa Masoud umefanywa na Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi baada ya mashauriano na chama cha ACT-Wazalendo. Masoud amewahi kuhudumu katika nafasi za ngazi za juu katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo mwanasheria Mkuu wa serikali.

''...Baada ya kushauriana na Chama cha ACT-Wazalendo, Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dkt Hussein Ali Mwinyi amemteua Mheshimiwa Othman Masoud Othman Sharif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar'', imeeleza sehemu ya taarifa kutoka Ikulu ya Zanzibar kuhusu uteuzi huo.

 

Masoud anatarajiwa kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo kesho tarehe 2 Machi.