Kiongozi wa genge lililowateka wanafunzi zaidi ya 300 auawa na mahasimu wake Nigeria

Muhtasari
  • Daudawa anadaiwa kutekeleza vitendo vya utekaji nyara wa mwezi Desemba katika jimbo la Katsina
  • Chini ya makubaliano ya Februari, Daudawa alisamehewa katika jimbo la Zamfara baada ya kusema alitubu na kukabidhi silaha zake kwa serikali

Kiongozi mashuhuri wa genge lililojihusisha na vitendo vya utekaji nyara wa wanafunzi zaidi ya 300 nchini Nigeria mnamo Desemba ameuawa na genge hasimu, maafisa wanasema.

Auwalu Daudawa aliripotiwa kuvamiwa wakati akijaribu kuiba kundi la ng'ombe kutoka kwa kundi lenye silaha katika jimbo la kaskazini magharibi la Zamfara.

Daudawa anadaiwa kutekeleza vitendo vya utekaji nyara wa mwezi Desemba katika jimbo la Katsina.

Alipewa msamaha kama sehemu ya makubaliano ya amani mnamo Februari lakini inasemekana alirudi kwenye genge lake mapema wiki hii.

Chini ya makubaliano ya Februari, Daudawa alisamehewa katika jimbo la Zamfara baada ya kusema alitubu na kukabidhi silaha zake kwa serikali.

Wanachama wa genge lake la wahalifu waliahidiwa makazi na Gavana wa jimbo Bello Matawalle, pamoja na msaada wa kusaidia kuboresha maisha yao.

Siku ya Ijumaa, Daudawa na washirika wengine wanne wa genge lake walipigwa risasi baada ya majibizano makali ya risasi katika msitu karibu na mpaka na Katsina, afisa wa eneo hilo aliliambia shirika la habari la AFP.

"Aliwaongoza watu wake kwenye harakati za kulipiza kisasi kifo cha wafuasi wake wawili na genge hasimu wakati wa uvamizi ulioshindwa katika moja ya kambi zake mwezi uliopita," afisa huyo aliongeza.

Utekaji nyara wa mamia ya watoto wa shule katika jimbo la Katsina mwezi Desemba, ambao ulidaiwa kuongozwa na genge la Daudawa, ulikuwa moja wapo ya uvamizi uliodaiwa kulenga kupata malipo ya kikombozi.

Wanafunzi hao waliungana tena na familia zao wiki moja baada ya kutekwa nyara.

Serikali baadaye ilisisitiza kuwa hakuna fidia iliyolipwa wakati huo,

Wavulana waliachiliwa baada ya mazungumzo na watekaji nyara.

Mhariri wa BBC barani Afrika, Will Ross, anasema habari za kifo cha Daudawa huenda zikaanzisha tena mjadala ikiwa mikataba inapaswa kufanywa na wahalifu hao maarufu.

Makundi kama hayo yamefanya utekaji nyara wa wanafunzi kuwa biashara yenye faida kubwa nchini Nigeria kwa sababu ya malipo ya fidia, mwandishi wetu anaongeza.

Watoto wa shule, pamoja na wafanyabiashara kadhaa na watu kadhaa wa kisiasa, wametekwa nyara kwa nyakati tofauti na kuachiliwa baada ya fidia kulipwa - ingawa sio kwa kiwango kilichoonekana mwezi Desemba, wakati wavulana zaidi ya 300 walitekwa nyara kutoka shule yao ya bweni nje kidogo ya Mji wa Kankara.

Kikundi cha wanamgambo wa Kiislam Boko Haram kilisema wakati huo kilikuwa kilitekeleza vitendo vya utekaji, na kwamba kiliajiri magenge ya eneo hilo kutekeleza shambulio hilo.

Boko Haram awali ililenga shule kwasababu ya upinzani ulionao dhidi ya elimu ya 'Kimagharibi' ambayo wanaamini inavunja miiko ya Uislamu. Jina la kundi hilo lina maana kuwa ''Elimu ya Magharibi ni haram''