Rais wa Somalia apunguza mamlaka ya Waziri Mkuu

Rais Farmajo pia alimshtumu waziri mkuu huyo kwa "kuchukua hatua za kizembe ambazo zinaweza kusababisha mgogoro wa kisiasa na kiusalama nchini" humo.

Muhtasari

• Katika tangazo kwenye mtandao wa Facebook, ofisi ya Rais Farmaajo ilisema imemvua waziri mkuu, Mohamed Hussein Roble, mamlaka yake ya kuteua mawaziri.

• Mzozo wa kisiasa kati ya rais na waziri mkuu wa Somalia juu ya uchaguzi uliocheleweshwa umechukua mkondo mpya.

Muhula wa Rais Mohamed Abdullahi Mohamed madarakani ulimalizika mnamo mwezi Februari lakini hakuna uchaguzi mpya ambao umefanyika
Muhula wa Rais Mohamed Abdullahi Mohamed madarakani ulimalizika mnamo mwezi Februari lakini hakuna uchaguzi mpya ambao umefanyika
Image: AFP

Wasiwasi wa kisiasa nchini Somalia unazidi kutokota baada ya Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed kusema kuwa amepunguza mamlaka ya Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble juu ya suala la uchaguzi.

Mzozo wa kisiasa kati ya rais na waziri mkuu wa Somalia juu ya uchaguzi uliocheleweshwa umechukua mkondo mpya.

Katika tangazo kwenye mtandao wa Facebook, ofisi ya Rais Farmaajo ilisema imemvua waziri mkuu, Mohamed Hussein Roble, mamlaka yake ya kuteua majukumu muhimu, pamoja na mawaziri.

Rais Farmajo pia alimshtumu waziri mkuu huyo kwa "kuchukua hatua za kizembe ambazo zinaweza kusababisha mgogoro wa kisiasa na kiusalama nchini" humo. Tofauti za kisiasa kati ya waziri mkuu na rais zilizidi kuwa mbaya zaidi hivi karibuni kufuatia kutoweka kwa afisa wa ujasusi wa kike, Ikran Talil.

Shirika la kijasusi la usalama wa taifa limesema kuwa afisa huyo ameuawa na kundi la Al Shabab, madai ambayo wanamgambo wamekanusha.

Waziri mkuu alitaka uchunguzi kufanywa kwa shirika lenyewe la kijasusi, hatua iliyopingwa na rais.

Wote, Rais na waziri mkuu walitangaza uteuzi tofauti, katika nyadhifa sawa za wizara ya usalama na shirika la ujasusi.