Rais Museveni atoa onyo kwa magaidi baada ya mlipuko kutokea Kampala

Muhtasari

•Hii ni baada ya watu ambao hawajajulikani kutega bomu jana usiku kwenye sehemu ya starehe moja yani 'Bar' ijulikanayo kwa jina la Digida eneo ambalo watu wanapokula nyama ya Nguruwe, Komambogo kitongoji cha Kampala.

Image: BBC

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye pia ni amiri jeshi mkuu amesema watawashughulikia magaidi wote wanaojaribu kuishambulia Uganda.

Hii ni baada ya watu ambao hawajajulikani kutega bomu jana usiku kwenye sehemu ya starehe moja yani 'Bar' ijulikanayo kwa jina la Digida eneo ambalo watu wanapokula nyama ya Nguruwe, Komambogo kitongoji cha Kampala.

Katika taarifa iliyotolewa na Rais Museveni kwenye mtandao wake amesema amefahamishwa na vikosi vya usalama kuwa watu 3 walikwenda kwenye bar hiyo baada hiyo na kuacha mfuko wa plastiki chini ya meza waliokuwa wamekaa, na baadaye kulipuka na kuua mtu mmoja na wengine watano kujeruiwa.

Museveni amesema ni kundi la magaidi lakini watawakamata wote na kutokomeza harakati zao.

MATANGAZO

Hivi karibuni serikali ya Uingereza ilitaadharisha Uganda kushambuliwa na magaidi, lakini tahadhali hiyo haikuelezea magaidi wanakwenda kushambulia wapi.

Pia serikali ya Ufaransa ilionya raia wake nchini Uganda kuacha kwenda sehemu za umma, kama vile bar, sehemu za Ibaada, usafiri wa umma na sehemu zinazopendwa na wageni kwa usalama kama wao.

Msemaji wa jeshi la polisi nchini Uganda Fred Enanga amesema jeshi la polisi wakishirikiana na vikosi vingine vya usalama wanaendelea na uchuguzi kuwatafuta waliohusika na shambulio hilo.

Inakumbukwa mwaka 2010 Uganda ilishambuliwa na magaidi wa Al Shababu wakati watu wakiangalia fainali ya kombe la dunia na kuua zaidi ya watu 70 kwenye uwanja wa raga wa Kyadondo na mgahawa wa Ethiopia Kabalagala.

Kuanzia hapo Uganda imekuwa katika hali ya tahadhali ya vitendo vya magaidi.

Ila watu wanahoji saa hizo zilikuwa za marufuku ya kutoka nje je, inakuwaje watu walikuwa wanakunywa pombe kwenye bar huku bar nyingine zikiwa zimefungwa kwasababu ya marufuku iliyokuepo tangu mwezi wa Machi mwaka jana 2020 kutokana na janga la uviko19.