Waziri Mkuu wa Ethiopia aapa kuongoza wanajeshi kwenye uwanja wa vita

Muhtasari

• Hatua hii ilikuja baada ya kamati kuu ya chama tawala cha Prosperity kukutana siku ya Jumatatu kujadili vita hivyo.

• Waziri wa ulinzi aliviambia vyombo vya habari vya ndani baada ya mkutano huo kwamba vikosi vya usalama vitaanza "hatua tofauti" kuhusu mzozo huo.

• TPLF limeunda muungano na vikundi vingine vya waasi likiwemo Jeshi la Ukombozi la Oromo (OLA) huku mzozo huo ukikaribia mji mkuu.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anasema sasa atawaongoza wanajeshi wake "kwenye uwanja wa vita" huku mzozo wa mwaka mzima ukiukaribia mji mkuu, Addis Ababa.

"Kuanzia kesho, tutakwenda mbele ili kuongoza vikosi vya ulinzi," Bw Abiy alisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye Twitter Jumatatu jioni.

"Wale wanaotaka kuwa miongoni mwa wazawa wa Ethiopia, ambao watasifiwa na historia, inukeni kwaajili ya nchi yenu leo. Tukutane mbele," aliongeza.

Hatua hii ilikuja baada ya kamati kuu ya chama tawala cha Prosperity kukutana siku ya Jumatatu kujadili vita hivyo.

Waziri wa ulinzi aliviambia vyombo vya habari vya ndani baada ya mkutano huo kwamba vikosi vya usalama vitaanza "hatua tofauti" kuhusu mzozo huo.

Tangu Novemba mwaka jana, serikali na vikosi vya waasi vya Tigray People’s Liberation Front (TPLF) vimekuwa vikishiriki katika vita vilivyoanzia Tigray na kuenea katika mikoa jirani ya Amhara na Afar.

TPLF limeunda muungano na vikundi vingine vya waasi likiwemo Jeshi la Ukombozi la Oromo (OLA) huku mzozo huo ukikaribia mji mkuu.

Wajumbe maalumu kutoka Umoja wa Afrika na Marekani wamekuwa wakijaribu kusuluhisha mzozo katika siku za hivi karibuni lakini kumekuwa na mafaniko madogo hadi sasa.

Mzozo huo umesababisha vifo vya maelfu ya watu, mamilioni ya watu wamelazimika kuondoka makwao na mamia ya maelfu wengine wanakabiliwa na njaa.