Mkurugenzi wa zamani wa gereza Rwanda afungwa kwa wizi

Muhtasari
  • Mkurugenzi wa zamani wa gereza Rwanda afungwa kwa wizi

Mahakama ya Rwanda imemhukumu kifungo cha miaka mitano jela aliyekuwa mkurugenzi wa gereza kuu la Kigali kwa kosa la kuiba pesa za mfungwa wa Uingereza.

Innocent Kayumba, ambaye alihukumiwa Ijumaa jioni pamoja na makamu wake wa zamani Eric Ntakirutimana, amekata rufaa dhidi ya hukumu hiyo, hati ya mahakama inaonyesha.

Mahakama ilimwachilia mfungwa mtaalamu wa IT ambaye alitumia ujuzi wake kudukua kadi ya Visa ya mwathiriwa baada ya kuambia mahakama kwamba alilazimishwa na mkurugenzi wa gereza kufanya hivyo.

Alisema alitakiwa “kuichambua” kadi iliyohifadhiwa na uongozi wa magereza baada ya kubaini kuwa akaunti ya benki iliyounganishwa nayo ilikuwa na kiasi kikubwa cha fedha.

Mfungwa huyo mwenye uraia wa Uingereza na Misri aliiambia mahakama kwamba zaidi ya £7,000 ($9,300) zilichukuliwa kutoka kwa akaunti yake kwa kutumia kadi yake mwaka jana bila yeye kujua.

Mahakama ilisema Bw Kayumba na naibu wake walipanga njama ya wizi huku mtaalamu wa IT akilazimishwa kuwafanyia kazi, hivyo hakupatikana na hatia.

Bw Kayumba, afisa mkuu wa kijeshi, alihamishwa hadi katika huduma za magereza mwaka wa 2014, akiongoza gereza moja magharibi mwa Rwanda kabla ya kuhamia gereza kuu la mji mkuu.

Alikamatwa mapema mwaka huu.

KWINGINEKO NI KUWA;

Covid: Marufuku ya usafiri ya Uingereza kwa Nigeria yatajwa kama ‘ubaguzi sa usafiri’

Vizuizi vya usafiri vya Uingereza vimekosolewa na Nigeria, baada ya nchi hiyo kuwekwa kwenye orodha ya nchi ambao raia wake watatakiwa kufuata masharti fulani ili kuingia Uingereza huku kukiwa na hofu juu ya aina mpya ya kirusi cha COVID 19 Omicron.

"Kinachotarajiwa ni mtazamo wa kimataifa, sio kuchagua," Sarafa Tunji Isola, balozi wa Nigeria nchini Uingereza, aliiambia BBC siku ya Jumatatu.

Pia alikariri maoni yaliyotolewa na mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye alielezea vikwazo vilivyowekwa kwa baadhi ya nchi za kusini mwa Afrika kama "vikwazo vya usafiri vya ubaguzi wa rangi".

Sheria mpya zilianza kutumika saa 04:00 GMT.

Inamaanisha kuwa wasafiri wanaofika kutoka Nigeria watahitajika kuingia karantini ya hoteli - kwa gharama zao - na kujitenga kwa siku 10.

"Marufuku ya kusafiri ni ya ubaguzi wa rangi kwa maana kwamba hatushughulikii janga," Bw Isola aliambia kipindi cha Today. "Tunakabiliana na janga. Kila tunapokuwa na changamoto lazima kuwe na ushirikiano."