Fungua vitabu vyako, na ufunge miguu yako-Waziri nchini Afrika Kusini awaambia wasichana wa shule

Muhtasari
  • Bi Ramathuba alitetea ujumbe huo, ambao alisema ulilenga wavulana pia
  • Waziri huyo wa afya wa jimbo la Limpopo alikuwa akitembelea shule ya upili ya Gwenane katika kitongoji cha Sekgakgapeng siku ya Jumatano

Waziri wa afya wa kikanda ameshutumiwa nchini Afrika Kusini kwa kuwaambia wasichana wa shule "fungueni vitabu vyenu na mfunga miguu yenu".

Phophi Ramathuba alitoa maoni hayo alipotembelea shule ya upili kwa nia ya kutoa uhamasisho kuhusu elimu ya ngono ili kupunguza viwango vya mimba za utotoni.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii walikosoa matamshi hayo na kuhoji kwa nini yanaelekezwa kwa wasichana pekee.

Bi Ramathuba alitetea ujumbe huo, ambao alisema ulilenga wavulana pia.

Waziri huyo wa afya wa jimbo la Limpopo alikuwa akitembelea shule ya upili ya Gwenane katika kitongoji cha Sekgakgapeng siku ya Jumatano kuadhimisha siku ya kwanza ya mwaka mpya wa masomo.

"Kwa mtoto wa kike ninasema: Fungua vitabu vyako, na ufunge miguu yako. Usifungue miguu yako, fungua vitabu vyako. Asante sana," aliwaambia wanafunzi.

Aliongeza kuwa wasichana walikuwa wakishawishiwa na wanaume wazee kwa kutumia anasa kama vile wigi za bei ghali na simu za mkononi.

Maoni hayo yalizua ukosoaji baada ya video ya hotuba hiyo kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

"Hii si njia mwafaka ya kuzungumza na watoto kuhusu unyanyasaji, ngono na ridhaa", mtumiaji mmoja wa mitandao ya kijamii aliandika.

Mwanasiasa wa upinzani Siviwe Gwarube aliyataja matamshi hayo kuwa ni matatizo makubwa.

"Hii ilikuwa fursa ya kuwa na mazungumzo ya maana na wanafunzi hawa kuhusu idhini... Badala yake unalaumiwa. Kuwawekea shinikizo lisilofaa kwa wasichana", alisema katika ujumbe kwenye Twitter.

Bi Ramathuba aliambia tovuti ya habari ya Afrika Kusini TimesLIVE kwamba taarifa yake imetolewa nje ya muktadha, na ilielekezwa kwa wavulana pia.

"Niliwaambia wavulana kuzingatia elimu yao na sio kulala na wasichana," alisema.

Aliongeza kuwa wapiga kura wake huko Limpopo "walithamini ujumbe".

"Walikuwa wakisema kuwa wanaogopa kusema mambo haya na walinishukuru kwa kusema ilivyo," alisema.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa karibu wasichana 33,400 walio chini ya umri wa miaka 17 walijifungua nchini Afrika Kusini mwaka 2020.

Shirika la Save the Children linasema ukosefu wa fursa ya kupata elimu ya kina ya ngono pamoja na huduma za afya ambazo ni nafuu na zinazofaa ni sababu kuu zinazochangia mimba za utotoni nchini Afrika Kusini.