Mzozo wa Urusi:Urusi inaweza kuanzisha mashambulizi ya kemikali nchini Ukraine - Ikulu ya Marekani

Muhtasari

"sote tunapaswa kuwa macho", Ikulu ya Marekani imesema.

 

Image: BBC

Urusi inaweza kuwa inapanga shambulizi la silaha za kemikali au za kibayolojia nchini Ukraine - na "sote tunapaswa kuwa macho", Ikulu ya Marekani imesema.

Katibu wa habari Jen Psaki alisema madai ya Urusi kuhusu maabara ya silaha za kibiolojia ya Marekani, na utengenezaji wa silaha za kemikali nchini Ukraine, yalikuwa ya upuuzi.

Aliyaita madai hayo ya uwongo kuwa ni "janja ya wazi" ya kujaribu kuhalalisha mashambulizi yaliyopangwa zaidi na yasiyochochewa.

Inakuja baada ya maafisa wa Magharibi kuonyesha wasiwasi sawa kuhusu mashambulizi mapya.

Walisema "wanajali sana" juu ya hatari ambayo vita vinaweza kuongezeka, na haswa uwezekano wa Urusi kutumia silaha zisizo za kawaida.

Hii ina uwezekano mkubwa inarejelea silaha za kemikali ingawa neno hilo pia linahusu silaha za nyuklia za mbinu (ndogo), silaha za kibayolojia na mabomu machafu.

"Tuna sababu nzuri ya kuwa na wasiwasi," ofisa mmoja wa Magharibi alisema.

Walisema hii kwa kiasi fulani ni kutokana na kile kilichoonekana katika maeneo mengine ambako Urusi imekuwa ikihusika - hasa Syria ambako silaha za kemikali zilitumiwa na washirika wake.

Bi Psaki alisema: "Sote tunapaswa kuwa macho kwa Urusi ikiwezekana kutumia silaha za kemikali au za kibaolojia nchini Ukraine, au kuunda operesheni ya uwongo ya bendera kwa kuzitumia - ni muundo wazi."

Mapema siku ya Jumatano, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba Urusi imetumia roketi za thermobaric nchini Ukraine. Roketi hizi pia hujulikana kama mabomu ya vacuum kwa sababu hunyonya oksijeni kutoka kwa hewa inayozunguka ili kutoa mlipuko wa joto la juu.

Hii inazifanya kuwa mbaya zaidi kuliko vilipuzi vya kawaida vya ukubwa sawa, na inaweza kuwa na athari mbaya kwa watu walionaswa kwenye eneo la mlipuko.

Hofu kuhusu utumiaji wa silaha za kemikali ilitokana na madai ya Urusi ambayo yanaweza "kuweka eneo hilo " kwa aina fulani ya madai ya shambulizi la "bendera ya uwongo"-la kusingizia maafisa wa Magharibi walisema.

Katika ujumbe wa Twitter, Ubalozi wa Urusi ulirejelea madai kwamba "hati zilizopatikana hivi karibuni" zilionyesha sehemu za silaha za kibaolojia zilitengenezwa katika maabara ya Ukraine - kwa ufadhili wa Idara ya Ulinzi ya Marekani

Marekani ilitupilia mbali madai hayo, ikisema ni "aina ya operesheni ya upotoshaji ambayo tumeona mara kwa mara kutoka kwa Warusi kwa miaka mingi nchini Ukraine na katika nchi zingine".

Maafisa wa Urusi na vyombo vya habari pia wamedai katika siku za hivi karibuni kwamba Ukraine ilikuwa inapanga kujenga kinachojulikana kama bomu chafu - ambayo inatawanya nyenzo za mionzi.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Urusi amedai Ukraine imekuwa ikitafuta silaha za nyuklia.

Wengine wanaamini kuwa Moscow inasukuma madai haya ili kutoa uhalali kwa umma wake kuhusu kwa nini iliivamia Ukraine. Lakini maafisa wa Magharibi pia wanahofia kuwa inaweza kutumika kama msingi wa tukio la "bendera ya uwongo".

Kwa mfano, Urusi inaweza kudai mtawanyiko wowote wa silaha zisizo za kawaida zilitoka kwa vituo vya Kiukreni au askari, au zilitumiwa kwanza na Ukraine. Hiyo inaweza kuhalalisha, kwa Moscow, matumizi ya baadaye ya silaha zisizo za kawaida na Urusi.

Afisa huyo wa Magharibi alisema hadithi kama hizo zilitoka Urusi kabla ya matumizi yao nchini Syria.

Kulikuwa na "dalili zingine pia", walisema - labda wakimaanisha aina fulani ya habari za ujasusi. "Ni wasiwasi mkubwa kwetu."

Mshirika wa Urusi, serikali ya Assad, ilitumia silaha za kemikali nchini Syria mara kadhaa dhidi ya raia.

Urusi pia inashutumiwa kwa kutumia silaha hatari za kuathiri neva - aina ya silaha ya kemikali - katika jaribio la mauaji kama yale ya Sergei Skripal huko Salisbury mnamo 2018 na dhidi ya kiongozi wa upinzani Alexei Navalny nchini Urusi mnamo 2020.

Shirika la kimataifa linalosimamia Mkataba wa Silaha za Kemikali - OPCW - linaelezea silaha ya kemikali kama kemikali inayotumiwa kusababisha kifo cha kukusudia au madhara kupitia sifa zake za sumu.

Matumizi yao yamepigwa marufuku chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu bila kujali shabaha halali ya kijeshi kwa sababu athari zake hazibagui asilia na zimeundwa kusababisha majeraha makubwa na mateso yasiyo ya lazima.