Mfahamu binadamu mwenye macho makubwa zaidi duniani

Sidney de Carvalho Mesquita anaripotiwa kuwa na macho yenye mduara wa milimita 18.2.

Muhtasari

• Sidney de Carvalho Mesquita almaarufu Tio Chico kutoka Brazil anashikilia rekodi ya ulimwengu ya binadamu mwenye macho makubwa sana.

•Sidney alisema hapo awali familia yake ilikuwa na wasiwasi kuwa huenda ni ugonjwa.

​​Sidney de Carvalho Mesquita
​​Sidney de Carvalho Mesquita
Image: Facebook// Guinness World Records

Nani angewahi kufikiria kwamba mtu angeingia kwenye Kitabu cha Rekodi za Dunia kwa kuwa na macho makubwa?

Jamaa mmoja anayejulikana kama Sidney de Carvalho Mesquita almaarufu Tio Chico kutoka Brazil anashikilia rekodi ya ulimwengu ya binadamu mwenye macho makubwa sana.

Inaaminika macho yake ina mduara wa milimita 18.2, takriban inchi 0.71 tofauti na macho ya binadamu wa kawaida, hali ambayo inaweza kumfanya kuyatoa macho yake nje  umbali wa takriban sentimita  mbili.

Inaripotiwa kuwa kadri muda unavyosonga ndivyo macho ya Tio Chico yanazidi kuwa makubwa zaidi na kuchomoza zaidi kuliko  ya wanadamu wenzake, jambo ambalo familia yake na marafiki wameshangazwa nalo.

Alipohojiwa, Tio Chico alifichua kuwa wakati ambapo ameyakondoa macho kisha kuyarudisha ndani huwa anapoteza uwezo wa kuona kwa sekunde kadhaa. Aidha alfichua aligundua ana mboni kubwa ya macho kuliko kawaida, akiwa na umri mdogo wa miaka tisa  alipokuwa akijitazama kwenye kioo.

Sidney alisema hapo awali familia yake ilikuwa na wasiwasi kuwa huenda ni ugonjwa, ila baadaye walikuja kukubali na kusema hali yake ilikuwa ujuzi wa kipekee.

"Talanta yangu hakika ni zawadi niliyopewa na anaifurahia." alisema.

Anasema anashukuru kwa hali aliyozaliwa nayo kwani ilimletea sifa na kumfanya kutambuliwa sio tu nchini Brazil bali ulimwenguni kote.