Iran: Wapenzi 2 wafungwa miaka 10 jela kwa kuoneshana mapenzi hadharani

Wapenzi hao wote wenye miaka 21 walionekana kwenye video wakioneshana mabaha barabarani, Iran ilisema hicho ni kitendo cha usherati.

Muhtasari

• Mwanadada huyo pia aiongezewa hatia zaidi za kupatikana bila baibui na hijab na alikuwa anaonesha kichwa chake hadharani kinyume na Sharia ya Kiislamu.

Raia wa Iran wakioneshana mapenzi hadharani
Raia wa Iran wakioneshana mapenzi hadharani
Image: The Independent//Screengrab

Bila shaka kama wewe ni mfuatiliaji wa karibu wa kanuni za mataifa mengi ya Kiislamu kwa maana ya mataifa kutoka Mashariki ya Kati na Asia, utagundua kwamba nchi hizo zina sheria kali sana dhidi ya wanawake na uvaaji wake hadharani

Jarida moja la kimataifa limeripoti kuwa mahakama ya nchini Iran mapema wiki hii iliwahukumu wapenzi wachanga miaka 10 jela kila mmoja kwa kuonekana wakicheza video ya kimapenzi hadharani barabarani.

Kulingana na jarida hilo, wawili hao wenye umri wa miaka 21, walishtakiwa kwa kupiga jeki mienendo ya ukahaba na usherati, jambo ambalo Sharia za Kiiislamu zinalichukulia kwa uzito mkali kama vile mataifa mengi ya magharibi yanachukulia suala la ugaidi.

Klipu hiyo ambayo ilisambazwa pakubwa kwenye mitandao ya kijamii ya Twitter na Tiktok inawaonesha wawili hao msichana na mvulana wakichezeshana kwa mahaba, huku kijana akimbeba hobela hobela mpenzi wake akipiga misele naye barabarani.

Kando na kupatikana na hatia ya ‘kueneza tabia za usherati’ mwanadada huyo pia alishtakiwa kwa kuonekana hadharani bila baibui, vazi ambalo watoto wa kike wa Kiiislamu huvaa ili kuficha vichwa vyao na sehemu ya nyuso zao wakiwa hadharani.

Kila mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka 10 na miezi sita jela na kupigwa marufuku kuondoka nchini humo, kwa mujibu wa Agence France-Presse (AFP) na BBC.

Haya yanajiri kipidni ambapo mamia ya watu wamekuwa wakiandamana kupinga unyanyasaji dhidi ya wanawake ambapo majarida ya kimataifa mwishoni mwa mwaka jana yaliripoti kuwa vyombo vya dola vilikuwa vikifyatua risasi moja kwa moja kwa wanawake waandamanaji, bunduki zao zikielekezwa kwenye nyuso na sehemu zao za siri.