Asafiri kwa ngamia kwa saa 7 ili kujifungua mtoto

Yeye na mumewe walimpa mtoto wao jina Jararh.

Muhtasari
  • Hospitali ya Bani Saad ndiyo kituo pekee cha afya kilichosalia katika mkoa wa Mahwit kaskazini magharibi mwa Yemen.

Siku za Mona zilipotimia na uchungu wa uzazi ulipoanza, ngamia alikuwa ndio tegemeo lake.

Mona mwenye umri wa miaka 19, kutoka nchini Yemen alifikiri kwamba ingemchukua saa 4 kusafiri kilomita 40 katika ardhi ya milima hadi kufikia hospitali, lakini ilimchukua saa 7 kutokana na kutokuwa na barabara, matatizo ya ujauzito, na hali mbaya ya hewa.

"Nilikuwa na maumivu makali kwa kila hatua ambayo ngamia alipiga," asema. Wakati hata ngamia hakuweza kuendelea, Mona alishuka na kukamilisha hatua ya mwisho ya safari yake kwa miguu na mumewe.

Hospitali ya Bani Saad ndiyo kituo pekee cha afya kilichosalia katika mkoa wa Mahwit kaskazini magharibi mwa Yemen.

Kutoka kijiji cha Mona cha Al-Makara, chaguo pekee ni kupanda ngamia au kutembea kwenye njia hatari ya mlima.

Mona, ambaye alikuwa ameshikilia ngamia wakati wa safari hii, alihofia maisha yake na ya mtoto mchanga tumboni mwake.

“Hiyo barabara ni ya mawe.Safari hiyo inakuchosha kimwili na kiakili,” anasema.

"Katika safari nzima, nilimwomba Mungu mara nyingi amwokoe mtoto wangu lakini aniepushe na maumivu haya makali."

Mona hakumbuki tulipofika hospitali, lakini anakumbuka kujawa na matumaini na furaha baada ya kusikia kilio cha mtoto.

Yeye na mumewe walimpa mtoto wao jina Jararh.