Mwanaume anusurika kifo kwa kujinasua kutoka kinywa cha mamba Australia

Marcus McGowan, mwenye umri wa miaka 51, ameeleza kwa kina jinsi alivyoweza kujinasua

Muhtasari
  • Alisafirishwa kwa ndege hadi hospitali ya kisiwa kilicho karibu, na baadaye akasafirishwa hadi Cairns kwa matibabu zaidi.

Mwanamume mmoja raia wa Australia amenusurika kifo baada ya kushambuliwa na mamba wa maji ya chumvi alipokuwa mapumzikoni katika hoteli moja huko Queensland.

Marcus McGowan, mwenye umri wa miaka 51, ameeleza kwa kina jinsi alivyoweza kujinasua kichwa chake kutoka kinywa cha mamba huyo lakini alipata majeraha.

Alisafirishwa kwa ndege hadi hospitali ya kisiwa kilicho karibu, na baadaye akasafirishwa hadi Cairns kwa matibabu zaidi.

Mashambulizi ya mamba si ya kawaida nchini Australia, lakini kumekuwa na ongezeko la visa kama hivyo katika miezi ya hivi karibuni.

Bw McGowan alisema alikuwa majini na kundi la watu yapata kilomita 28 (maili 17.3) kutoka Kisiwa cha Haggerstone karibu na Cape York alipoumwa kwa nyuma.

"Nilidhani ni papa lakini nilipofika juu, niligundua kuwa ni mamba. Niliweza kufungua taya zake kwa umbali wa kutosha kunitoa kichwa," alisema katika taarifa.

Mamba - anayeshukiwa kuwa mchanga - alirudi kwa safari nyingine, alisema, lakini aliweza kumsukuma, akiuma mkono wake.

Idara ya mazingira ya Queensland inasema itachunguza tukio hilo, lakini "mamba katika bahari ya wazi wanaweza kuwa wagumu kuwapata kwani wanyama hao mara nyingi husafiri makumi ya kilomita kwa siku".

KWINGINEKO NI KUWA;

Afrika Kusini yatia saini kinga ya kidiplomasia kabla ya mkutano wa BRICS

Afrika Kusini imetia saini kinga ya kidiplomasia kwa maafisa wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tano zenye uchumi unaokua kwa haraka - BRICS na mkutano wa kilele utakaofanyika mwezi Agosti.

Hii inafungua milango kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhudhuria, baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), kutoa hati ya kukamatwa kwake inayohusiana na uhalifu dhidi ya binadamu kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Ziara iliyopangwa kufanywa na Rais wa Urusi Vladimir Putin nchini Afrika Kusini kwa mara nyingine tena imeiweka nchi hiyo katikati ya utata kuhusu wajibu wa kumkamata rais ambaye bado yuko madarakani.

Idara ya uhusiano wa kimataifa ya Afrika Kusini ilichapisha katika gazeti rasmi la serikali siku ya Jumatatu ikitambua mikutano miwili ambayo itakuwa na kinga ya kidiplomasia.

Hii ni pamoja na mkutano wa 15 wa kilele wa BRICS utakaofanyika Johannesburg mwezi Agosti.