Magenge ya Haiti yateketeza vituo vya polisi

Machafuko hayo yamelemaza usafiri wa anga, jambo ambalo limezuia kurejea kwake.

Muhtasari
  • Magenge yanayoshinikiza kuondolewa madarakani kwa Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry yamechoma moto vituo vya polisi katika mji mkuu wa Port-au-Prince.
Zaidi ya watu 15,000 wamekimbia makazi yao katika wiki iliyopita kutokana na ghasia hizo.
Zaidi ya watu 15,000 wamekimbia makazi yao katika wiki iliyopita kutokana na ghasia hizo.

Magenge yanayoshinikiza kuondolewa madarakani kwa Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry yamechoma moto vituo vya polisi katika mji mkuu wa Port-au-Prince.

Kituo cha polisi kilicho katika soko la wazi la Salomon ndicho cha hivi punde zaidi kulengwa, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

Magenge katika mji huo uliokumbwa na ghasia yalizidisha mashambulizi yao wakati Bw Henry alipoondoka kwa mkutano wa kilele wa kanda wiki jana.

Machafuko hayo yamelemaza usafiri wa anga, jambo ambalo limezuia kurejea kwake.

Bwana Henry alijaribu kusafiri hadi Port-au-Prince siku ya Jumanne lakini badala yake akaishia katika eneo la Marekani la Puerto Rico.

Hakuweza kutua katika mji mkuu wa Haiti kwa sababu uwanja wake wa ndege wa kimataifa ulifungwa huku wanajeshi wakizuia majaribio ya watu wenye silaha kutaka kuuteka.

Mamlaka ya usafiri wa anga katika nchi jirani ya Jamhuri ya Dominika pia iliirejesha ndege ya waziri mkuu, ikisema kwamba hawakupewa mpango unaohitajika wa safari.

Bw Henry hajatoa taarifa yoyote kwa umma tangu alipozuru Kenya, ambapo alikuwa akijaribu kuokoa makubaliano ya nchi hiyo ya Kiafrika kuongoza vikosi vya mataifa mbalimbali kusaidia kurejesha utulivu nchini Haiti.

Magenge katika mji mkuu walichukua fursa ya kutokuwepo kwake kuanzisha mfululizo wa mashambulizi yaliyoratibiwa.