Msichana 16, akamatwa kwa kumuua binamuye, Siaya

Mshukiwa alichukuwa mkuki nyumbani kwao na kuwarushia watoto wengine na kumdunga kichwani mtoto wa miaka tisa ambaye alikufa papo hapo.

Muhtasari

• Mshukiwa ambaye ni mgonjwa wa akili alikuwa akicheza ndani ya boma lao na watoto wengine wadogo.

 

Picha ya maktaba ya gari la Polisi katika eneo la uhalifu.
Image: MAKTABA

Polisi katika Kaunti ya Siaya wanachunguza kisa ambapo msichana mwenye umri wa miaka 16 anadaiwa kumuua mpwawe wa umri wa miaka 9 kwa kutumia mkuki katika kijiji cha Nyandiwa katika kaunti ndogo ya Alego/Usonga.

Naibu Chifu wa Nyandiwa Joseph Otieno Aloo aliripoti kwa Kituo cha Polisi cha Siaya kwamba kulikuwa na tukio la mauaji katika kijiji cha Nyandiwa.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Siaya Cleti Kimaiyo, maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Siaya walifika eneo la tukio na kubaini kuwa mshukiwa ambaye ni mgonjwa wa akili alikuwa akicheza ndani ya boma lao na watoto wengine wadogo.

Alieleza kuwa ghafla kulitokea kutoelewana kati yao kabla ya mtuhumiwa kuingia nyumbani kwa baba yake na kuchukuwa mkuki ambao aliwarushia watoto wengine na kumdunga kichwani mtoto wa miaka tisa ambaye alikufa papo hapo.

Akithibitisha kisa hicho, Bw. Kimaiyo alisema eneo la tukio lilishughulikiwa na kurekodiwa kabla ya mwili huo kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Siaya huku uchunguzi kuhusu kisa hicho ukiendelea.

Mshukiwa alikamatwa na anasaidia polisi katika uchunguzi. Silaha ya mauaji pia ilipatikana na kuwekwa kama ushahidi.