Ruto asema Ngilu anayo nafasi bora nchini Kenya

Rais aliwataka viongozi wote wanawake kuendeleza ushauri waliopewa na Mama Ngilu kwa kizazi kijacho cha viongozi.

Muhtasari

• Ngilu alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwakilisha eneo bunge la Kitui ya kati mwaka wa 1992 na kuhudumu katika eneo bunge hilo hadi 2013.

Rais William Ruto akisalimiana na aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu wakati wa uzinduzi wa kikao cha Wanawake cha Baraza la Magavana mnamo Machi 7, 2024. Picha: PCS
Rais William Ruto akisalimiana na aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu wakati wa uzinduzi wa kikao cha Wanawake cha Baraza la Magavana mnamo Machi 7, 2024. Picha: PCS

 Rais William Ruto amesema kwamba aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu anachukua nafasi maalum katika historia ya Kenya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Magavana Wanawake wanaojiita G7, Ruto alisema ni kwa sababu alikuwa mwanamke wa kwanza wa Kenya kuthubutu kuwania urais. Aliendelea kusema kwamba moyo wake wa kuthubutu uliwatia moyo wanawake wengi ambao ni viongozi leo.

Rais aliwataka viongozi wote wanawake kuendeleza ushauri waliopewa na Mama Ngilu kwa  kizazi kijacho cha viongozi.

"Ngilu anashikilia nafasi maalum katika nchi yetu. Yeye ndiye mwanamke wa kwanza kuthubutu kuwania urais. Charity mara nyingi huwa mgumu kwangu lakini ni msukumo mkubwa kwa wanawake wengi kote nchini Kenya. Moyo wake wa kuthubutu umewatia moyo wengi wenu," Ruto alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alimmiminia sifa gavana huyo wa zamani wa Kitui kwa kuwachochea wanawake wengi kuingia katika uongozi nchini Kenya. Sakaja alisema kuwa Ngilu alijitokeza kuwa kinara wa matumaini kwa viongozi wengi wa kike.

"Asante kwa kuandaa njia kwa uongozi wa wanawake nchini Kenya. Kama si nyinyi, magavana wengi wa kike hawangekuwa na ujasiri wa kujiunga na siasa," alisema.

Ngilu alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwakilisha eneo bunge la Kitui ya kati mwaka wa 1992 na kuhudumu katika eneo bunge hilo hadi 2013. Katika uchaguzi mkuu wa 1997, Ngilu alitaka kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Kenya kwa tiketi ya Social Democratic Party of Kenya, akimaliza wa tano nyuma ya aliyekuwa mshindi, marehemu Rais Daniel Moi.

Baadaye, alijiunga na Chama cha  National Party of Kenya. Katika uchaguzi mkuu wa Desemba 2002, chama chake kilikuwa sehemu ya Muungano wa Kitaifa wa National Rainbow Coalition (NARC).

Muungano huo ulishinda uchaguzi wa 2002, na Rais Mwai Kibaki akamteua kuwa Waziri wa Afya alipotaja Baraza lake la Mawaziri tarehe 3 Januari 2003. Pia aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa NARC.

Ngilu alihudumu kama Waziri wa Afya kutoka 2003 hadi 2007 na Waziri wa Maji na kutoka Aprili 2008 hadi 2013. Pia alikuwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji kutoka 2013 hadi 2015. Mnamo 2017, alimshinda Julius Malombe na kuwa gavana wa Kitui. Yeye, hata hivyo, hakutetea kiti hicho mnamo 2022.