Familia yalilia haki baada ya mwanao aliyehusishwa na jamii ya wasagaji na mashoga kubakwa na kuuawa Nyeri

Muhtasari

Kulingana na babake John Lumumba, polisi walikuwa wakiwazungusha kuhusiana na mauaji ya bintiye aliyekuwa akifanya kazi katika mji wa Karatina.

Familia hiyo kutoka Naivasha ilibaini kuwa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na mauaji ya msichana ambaye alihusishwa kwa karibu na jamii ya wasagaji, mashoga, watu wa jinsia mbili na waliobadili jinsia (LGBT).

Mauaji hayo yalizua mdahalo mkali kwenye mitandao ya kijamii na wito wa kuheshimu jamii ya LGBT ambayo imekabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya watu.

Millicent Oloo (kushoto) mama wa Sheila Adhiambo Lumumba akifarijiwa na rafiki yake nyumbani kwake.
Millicent Oloo (kushoto) mama wa Sheila Adhiambo Lumumba akifarijiwa na rafiki yake nyumbani kwake.
Image: George Murage

Familia ya Sheila Adhiambo mwenye umri wa miaka 24 ambaye alibakwa na genge na kuuawa wiki jana huko Karatina Nyeri katika mazingira ya kutatanisha inawashutumu polisi kwa kuwazungusha.

Familia hiyo kutoka Naivasha ilibaini kuwa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na mauaji ya msichana ambaye alihusishwa kwa karibu na jamii ya wasagaji, mashoga, watu wa jinsia mbili na waliobadili jinsia (LGBT).

Wiki iliyopita, watu wasiojulikana walivamia nyumba ya mwathiriwa, kumbaka na kumuua kwa madai kuwa alikuwa msagaji.

Ziara ya familia hiyo mjini Karatina haikuzaa matunda yoyote walipohamisha mwili wa marehemu hadi katika hifadhi ya maiti ya kaunti ndogo ya Naivasha kabla ya mazishi.

Shirika la Amnesty International katika ukurasa wake wa Twitter limelaani mauaji hayo na kuapa kusimama na familia likishikilia kuwa hakuna mtu anayefaa kutendewa unyama kama huo.

"Tunasimama pamoja na familia ya Sheila Adhiambo Lumumba wakati wa majonzi na tutafuatilia suala hili hadi haki ipatikane," inasema nukuu hiyo.

Kulingana na babake John Lumumba, polisi walikuwa wakiwazungusha kuhusiana na mauaji ya bintiye aliyekuwa akifanya kazi katika mji wa Karatina.

Akizungumza katika nyumbani kwao huko Naivasha, Lumumba alisimulia uchungu wao wakitafuta haki  huku washukiwa kadhaa wakikamatwa na baadaye kuachiliwa.

"Alikufa kifo cha uchungu sana kwani nyumba yake na vyombo vya kibinafsi vilikuwa vimeowa damu ikimaanisha alivuja damu nyingi kabla ya kufa," alisema siku ya Jumatano.

Aliongeza kuwa uchunguzi wa maiti uliofanyika kwenye mwili huo ulionyesha kuwa marehemu alifariki baada ya kupigwa na kifaa butu kichwani na kuongeza kuwa alikuwa na majeraha ya kuchomwa shingoni na machoni.

Mamake Millicent Oloo alitaja mauaji hayo kuwa chungu zaidi kuwahi kutokea kwa familia hiyo.

"Binti yangu alikufa kifo cha uchungu sana kwani nyumba yake ilikuwa imetapakaa damu na tunatoa wito kwa polisi kuwakamata waliohusika na kitendo hiki cha kinyama," alisema.

Mauaji hayo yalizua mdahalo mkali kwenye mitandao ya kijamii na wito wa kuheshimu jamii ya LGBT ambayo imekabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya watu.